Dili la Miquissone, Simba lanoga!

HUKO mtaani, mashabiki wa Simba wanaliimba jina la nyota wa zamani wa timu hiyo, Luis Miquissone wakitaka arejeshwe, kisi cha kuwafanya mabosi wa klabu hiyo kukuna kichwa na kupiga hesabu ndefu za kumrejesha hasa baada ya kupata baraka za kocha Roberto Oliveira aliyemkubali.

Kocha Robertinho amekubali ubora wa mshambuliaji huyo aliyeuzwa Al Ahly ya Misri mwanzoni mwa msimu uliopita, lakini inaelezwa kwa sasa mabosi wa Simba wakuna kichwa kutokana na ishu ya fedha.

Luis ambaye klabu yake ya sasa Al Ahly jana ilikuwa uwanjani kucheza mechi ya kwanza ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya watetezi, Wydad Casablanca ya Morocco, amewekwa sokoni akiuzwa kwa klabu itakayofikia dau inaloitaka klabu hiyo ya Misri.

Katika kumweka sokoni, Simba ndio klabu iliyopewa kipaumbele cha kwanza kuuliziwa kama itamhitaji kutokana na mkataba wake wakati anauzwa kwa Waarabu hao akitokea kwa wekundu wa Msimbazi.

Simba tayari imeshazungumza mara kadhaa na nyota huyo wa Msumbiji ambaye amewataka mabosi wa Simba kufika kwenye dau la Dola 20,000 (Sh47.3 milioni) kwa mwezi ili arejee nyumbani.

Dau hilo linaonekana kuwapasua vichwa mabosi wa Simba ambao walikuwa tayari kufumba macho kumpa mshahara wa Dola 10,000 (Sh24 milioni) kwa mwezi ikiwa ni nusu ya fedha aliyotaka winga huyo wa kazi.

Simba mapema waliamua kumshirikisha Robertinho juu ya hatua hiyo na kiwango cha winga huyo ambapo Mbrazil huyo aliwaambia  mabosi wake; 'Nileteeni mtu wa kazi huyo.'

"Mshahara huo anaoutaka ni mkubwa kwa klabu zetu hapa, ingawa tunaheshimu na kutamani sana arudi lakini bado tunapambana naye kuangalia kama atarudi chini na kutusikiliza," kilisema chanzo makini kutoka ndani ya Simba.

Mtihani mwingine wa Simba ni jinsi gani itamalizana na Al Ahly inayohitaji kiasi kisichopungua Dola 250,000 (Sh592 milioni) ili wamuachie Luis ambaye bado ana mkataba na Waarabu hao.

Kwa sasa Luis hayupo kwenye hesabu za Al Ahly kwa msimu huu na tayari kocha wao Marcel Koller raia wa Uswisi ameshindwa kukubaliana kiwango cha winga huyo.

Hata hivyo, upande mwingine Simba inapiga hesabu kuwa kama watashindwana na Luis basi irudi sokoni kuangalia chaguo lao la pili kufanikisha usajili wa kushusha winga mwenye kasi, huku Kramo Aubin wa Asec Mimosas ya Ivory Coast na Makabi Lilepo wa Al Hilal ya Sudan wakitajwa.