Prime
Dili la Diarra kutimka Yanga lipo hivi!

Muktasari:
- Iko hivi. Kaizer Chiefs ilikuwa na hesabu za kumsajili Diarra baada ya makocha wa timu hiyo wakiongoza na Nasreddine Nabi kuhitaji kipa mpya wa boli ili timu hiyo ianze kutengeneza mashambulizi kuanzia nyuma.
PENGINE taarifa hii itawashusha presha mashabiki wa Yanga, wanaoianza wiki ya kwanza ndani ya Juni, baada ya kubainika kuwa, lile dili la kipa namba moja wa timu hiyo, Djigui Diarra anayetakiwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini limeota mbawa baada ya kuondolewa rasmi katika hesabu za mabosi.
Iko hivi. Kaizer Chiefs ilikuwa na hesabu za kumsajili Diarra baada ya makocha wa timu hiyo wakiongoza na Nasreddine Nabi kuhitaji kipa mpya wa boli ili timu hiyo ianze kutengeneza mashambulizi kuanzia nyuma.
Katika mapendekezo ya benchi hilo la ufundi, jina la Diarra lilikuwamo akibebwa na kumbukumbu ya kufanya kazi na Nabi aliyemsajili Yanga wakati akiifundisha timu hiyo na kufika nao fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ilipopoteza kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria.
Hata hivyo, taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo ni kwamba mabosi wa Kaizer wameliondoa jina la Diarra baada ya kupata uhakika wa muda uliosalia wa mkataba alionao na Wanajangwani.
Kaizer wakati inampigia hesabu Diarra ilijua kwamba kipa huyo amebakiza mkataba wa mwaka mmoja, lakini mabosi wa klabu hiyo wamejiridhisha kupitia Yanga kwamba kipa huyo raia wa Mali amebakiza mkataba wa miaka miwili ambapo inaona wazi haitakuwa rahisi klabu yake kumuachia.
“Diarra kuna mapendekezo yalikuja ili tumpate, lakini kwanza tuliambiwa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba alionao na Yanga, tukaona itakuwa rahisi kuzungumza na viongozi wake,” alisema bosi huyo wa juu ndani ya Kaizer na kuongeza;
“Tulipowatafuta wenzetu wa Yanga kwa kuwa ni rafiki zetu sio tu, walituambia walituonyesha hadi mkataba wenyewe ulivyo na kwamba umebakiza miaka miwili kumalizika, kwa hiyo unaona namna itakuwa ngumu kumpata kwa bei rahisi.
“Tunaweka nguvu kwenye machaguo mengine ambayo tulikuwa nayo, lakini uhakika ni kwamba hatutaweza kuendelea na dili hilo la Diarra ni kipa mzuri ila bajeti inatuzuia.”
Mbali na sababu hiyo inaelezwa Kaizer imepokea ushauri kutoka kwa kocha Nabi ya kwamba waachane na mpango wa kuchukua mchezaji kutoka Yanga kwa kuwa hataki kubomoa timu yake hiyo ya zamani.
Inaelezwa kwa sasa Kaizer inapambana kunasa nyota wawili kuitoka Simba, Joshua Mutale na Jean Charles Ahoua.
“Unajua tuna kocha mstaarabu sana (Nabi), ukiacha hilo la mkataba naona ameshauriana na wenzake na kuamua kuachana na hatua ya kuchukua mchezaji yeyote kutoka Yanga ambako alifanya kazi, hataki kuona anaibomoa timu yake ya zamani,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Ametuambia kwenye masisha yake hajawahi kurudi nyuma na kuchukua mchezaji kwenye ile klabu aliyotoka, anatamani kufanya kazi na wachezaji wake wa zamani lakini hapendi kuwa chanzo cha kubomoa sehemu aliyojenga.”
Inaelezwa kwa sasa Kaizer inapambana kunasa nyota wawili kuitoka Simba, Joshua Mutale na Jean Charles Ahoua waliovutiwa nao kupitia mechi mbili ilizocheza timu hiyo dhidi ya Singida Black Stars, ikiwamo ya Ligi Kuu iliyoshinda 1-0 na ile iliyopoteza kwa 3-1 katika Kombe la Shirikisho (FA).