Coastal Union waitana Tanga

Muktasari:
- Uongozi huo umeitisha mkutano mkuu maalumu utakaofanyika Julai 12 kujadili taarifa ya maendeleo ya klabu hiyo kwa msimu huu na mipango ya maandalizi ya msimu mpya ili kuweka mambo sawa na kuepuka kuishi kwa wasiwasi kama ilivyokuwa msimu huu ambapo klabu inapambana isicheze mechi za mtoano (play-off).
WAGOSI wa Kaya ‘Coastal Union’ wanajiandaa kuzipokea timu za Fountain Gate na Tabora United katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara za kufungia msimu huu, lakini mabosi wa klabu hiyo wamewaita wanachama ili kujadili mipango kwa maandalizi ya msimu mpya wa 2025-2026.
Uongozi huo umeitisha mkutano mkuu maalumu utakaofanyika Julai 12 kujadili taarifa ya maendeleo ya klabu hiyo kwa msimu huu na mipango ya maandalizi ya msimu mpya ili kuweka mambo sawa na kuepuka kuishi kwa wasiwasi kama ilivyokuwa msimu huu ambapo klabu inapambana isicheze mechi za mtoano (play-off).
Mkutano huo maalumu wa Coastal ambayo kesho itakuwa wenyeji wa Fountain Gate kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga utafanyika kwenye ukumbi wa Tanga Beach Resort jijini humo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mtendaji Mkuu wa Coastal, Omari Ayoub alisema katika mkutano huo ajenda nyingine ni kujadili mapato na matumizi, kutoa mrejesho wa mipango ya klabu kwa wanachama wa klabu hiyo ambao amewataja kuwa ndio mabosi wao na mipango ya msimu ujao.
“Ni mkutano ambao unafanyika kila mwaka na mwaka wetu wa msimu huwa unatamatika Juni, hivyo tunatarajia kukutana kujadili mapato na matumizi ya msimu uliopita lakini mipango mikakati ya msimu ujao,” alisema Ayoub na kuongeza”
“Coastal ni timu ya wanachama, hivyo tunarudisha kile kilichofanyika kwao lakini pia tunakutana kujadili mipango mipya ya msimu ujao. Naamini ni mkutano wa kawaida ambao unatambulika kikanuni.”
Mkutano uliopita Coastal Union mipango na mikakati yake ilikuwa ni kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kama ilivyokuwa msimu uliopita ilipokata tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu ambako ilitolewa raundi ya awali na Bravo do Marquis ya Angola, lakini mambo yameenda kombo ikishika nafasi ya 10 kwenye ligi ikiwa na pointi 31.
Kwa sasa timu hiyo inapambana kuepuka kucheza mtoano ikisikilizia mechi mbili zilizosalia za kufungia msimu ikiwamo ya kesho na ile ya Juni 22 itakapoialika Tabora United, na kama itashinda mechi zote itajiweka salama kwani itafikisha pointi 37 ilizonazo Tabora United kwa sasa.