Clara Luvanga aandika historia mpya Saudia

Muktasari:

  • Clara bado anaongoza kwenye orodha ya wafungaji akiweka nyavuni mabao 11 na kutoa asisti tano na huenda kama ataendelea kucheza na kufunga anaweza kuibuka na kiatu cha dhahabu akiwaacha baadhi ya nyota kama Ibtisam Jraidi wa Al Ahli mwenye mabao 10.

MTANZANIA Clara Luvanga jana ameandika historia ya kubeba kombe la kwanza la ligi nchini Saudia akiwa na timu yake ya Al Nassr iliyotetea ubingwa mbele ya Al Hilal kwa kuichapa mabao 4-2.

Kwenye mchezo huo wa dabi, Clara alifunga bao moja na kutoa asisti mbili za mabao zilizofungwa na Sara Al Hamad, Lina Boussaha na Mubarkh Al Saiari.   

Huu unakuwa ubingwa wa kwanza kwa Clara tangu aanze soka kwani hakufanikiwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya wanawake nchini Tanzania akiwa na Yanga Princess.

Al Nassr imecheza mechi 11 na imebakiza michezo mitatu ili kukamilisha ratiba ya michezo 14 na imechukua ubingwa baada ya kuongoza kwa pointi 31 ikitofautiana pointi 13 na Al Shabab iliyopo nafasi ya pili na pointi 18.

Mbali na hivyo, Clara bado anaongoza kwenye orodha ya wafungaji akiweka nyavuni mabao 11 na kutoa asisti tano na huenda kama ataendelea kucheza na kufunga anaweza kuibuka na kiatu cha dhahabu akiwaacha baadhi ya nyota kama Ibtisam Jraidi wa Al Ahli mwenye mabao 10.

Kwa ubingwa huo inawafanya Clara na chama lake kupata nafasi ya kushiriki hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa barani Asia msimu ujao wa 2024-25 wakati michuano hiyo itakapofanyika kwa mara ya kwanza kwa wanawake baada ya misimu minne ya mashindano ya klabu Asia ambayo timu zimekuwa zikishikiri kwa kualikwa. Msimu huu tayari imevuka hatua ya 16 bora kwa kuifunga Shabab Al- Ahli kwa jumla ya mabao 4-2.

Wakati Clara anafurahia ubingwa, mambo yanaweza kuwa mabaya kwa Mtanzania mwenzake Enekia Lunyamila ambaye chama lake la Eastern Flames jana lilichapwa mabao 8-0 na Al Ahli na kuendelea kusalia nafasi ya saba kati ya timu nane zinazoshiriki ligi hiyo.

Ligi ya Saudia ni timu moja tu ndio inayoshuka daraja na kama Flames itasalia nafasi ya saba kuna uwezekano wa kusalia kwenye ligi msimu ujao.

RONALDO ALIWABEBA 2023
Unaambiwa msimu uliopita, wakati timu hiyo ikiwa haijawahi kutwaa ubingwa wa ligi hiyo ya wanawake, supastaa wa timu hiyo kwa upande wa wanaume, Cristiano Ronaldo, aliwatembelea wachezaji mazoezini na kuwapa hamasa, jambo ambalo hawakulitarajia.

Ronaldo, ambaye anachezea timu ya Al Nassr ya wanaume katika Ligi Kuu ya Saudia, alitembelea mazoezi ya timu hiyo ya wanawake na kuzungumza na wachezaji na kuwapa hamasa ya kupambana hadi wabebe taji hilo. Ronaldo anafahamika kwa njaa yake isiyoisha ya kusaka mafanikio na uwapo wake ukawahamasisha wachezaji wa timu hiyo kwa mujibu wa kocha wao.

"Siri ya kutwaa taji hili kwa mara ya kwanza ni uwapo wa nahodha Ronaldo kwenye mazoezi na akazungumza na wachezaji," kocha wa timu ya wanawake ya Al-Nassr, alisema kupitia Timeline CR7.

Mbali na kuzungumza na wachezaji, Ronaldo aliposti ziara yake hiyo ya hamasa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii wakati timu hiyo ikiwa imebakiza mechi mbili kumaliza msimu. Ikatwaa ubingwa huo ikiwa na pointi 35, tatu juu ya mahasimu wao wa karibu Al Hilal. Hivyo hili ililotwaa mwaka huu ni taji lao la pili mfululizo.