Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Cheki mke alivyomfilisi Emmanuel Eboue

MIAKA 11 iliyopita alikuwa akipata namba katika klabu kubwa kabisa na kucheza mechi kubwa zenye hadhi ya kutazamwa na dunia nzima.

Hiki kilikuwa kipindi chake cha miaka saba kwenye Ligi Kuu England, alivuna mamilioni ya pesa kama malipo ya mishahara yake na aliishi kwenye mahekalu na kuendesha magari ya kifahari.

Lakini, kwa sasa beki wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Eboue, anaishi kama digidigi, wakati mwingine analala tu kwenye vibaraza vya nyumba za marafiki zake, hata nguo zake anafua mwenyewe kwa mikono, hana tena zile mashine za kufulia.

Staa huyo mwenye umri wa miaka 34 anasimulia yote na kuweka hadharani namna utajiri wake wote ulivyokwisha na kuwa masikini kiasi cha kumfanya akaribia kujiua.

“Mungu anisaidie tu,” anasema.

“Anisaidie tu kuondoa haya mawazo mabaya kwenye akili yangu.”

Eboue ameamua kuweka bayana kila kitu ili kuwaamsha wengine wasiingie katika njia alizopita yeye ambazo zimemgharimu kwa kiasi kikubwa. Eboue wa sasa ni kama anasumbuliwa na matatizo ya akili kutokana na kuathirika kisaikolojia na namna alivyopoteza mali zake zote.

Alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Arsenal na aliichezea timu hiyo kwa mafanikio makubwa hata kwenye ile fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona mwaka 2006. Arsenal ilifungwa, lakini Eboue aliendelea kuwa shujaa wa Arsenal. Alikuwa muhimu pia katika timu yake ya taifa ya Ivory Coast. Lakini, furaha zote hizo za wakati huo zimekuwa majonzi, zimekuwa machozi. Eboue kwa sasa hawezi kucheza mpira kutokana na hali yake na hilo limekuwa zito kweli kulikabili. Eboue kwa sasa amepoteza kila kitu na sababu kubwa ya jambo hilo ni talaka yake kwa mkewe Aurelie. Mwanamke huyo sasa ndiye mmiliki wa kila kitu.

Hata mawasiliano na mabinti zake; Clara (14) na Maeva (12) na mtoto wake wa kiume Mathis (9), yamekatika. Zile wiki tatu za kutakiwa kuliachia jumba la huko London zimeshapita.

Jumba hilo alilokuwa akiishi na mkewe huyo, Jaji, atasaini uhamisho wa umiliki wake kwa mke wake kama Eboue hatafanya hivyo mwenyewe.

Staa huyo aliishi kwenye jumba hilo kwa furaha kubwa na familia yake, kabla ya kulinunua kabisa, lakini sasa Aurelie ameamua kuliweka sokoni.

Anachofahamu Eboue ni kwamba mkewe atapangisha tu jumba hilo. Kwa sasa vitu vyake vyote vilivyokuwa kwenye jumba hilo vimeshawekwa kwenye mabegi, kinachosubiriwa ni muda tu wa kuambiwa abebe kila kilicho chake aondoke.

“Kwa sasa sina pesa ya kuendelea kuwa na Mwanasheria. Nipo kwenye ile nyumba, lakini nimekuwa na mashaka makubwa. Kwa sababu ni muda gani polisi watakuja kunitimua. Wakati mwingine nazima taa kwa sababu sitaki watu wafahamu kama nipo ndani. Najaza vitu kibao mlangoni. Nyumba yangu mwenyewe, niliyohangaika sana kupata pesa za kuinunua, lakini sasa naishi kwa wasiwasi. Siwezi kuuza nguo zangu au mali nyingine nilizonazo. Nitapambana hadi mwisho kwa sababu hii siyo haki kabisa,” anasema Eboue.

Eboue alivuna pesa za kutosha huko Arsenal na alikuwa akilipwa zaidi ya Pauni 1.5 milioni kwa mwaka alipokuwa kwenye kikosi cha Galatasaray. Matumaini yake ya kurudi kwenye Ligi Kuu England alipotakiwa na Sunderland yaliyeyuka mwaka jana baada ya kukumbana na adhabu ya Fifa ya kufungiwa miezi 12 kutokana na kuwa na matatizo na wakala wake wa zamani. Eboue amesema hakuwa amefundishwa kabisa namna ya kusimamia pesa zake. Amesema mkewe ndiye aliyekuwa akisimamia kila kitu na kwamba yeye hakuwa mwangalifu sana kuhusu pesa. Amedai pia alikuwa amejiweka karibu na watu ambao walikuwa wakimpa ushauri wa ovyo uliomfanya apoteze pesa nyingi.

Kwa sababu hakuwa na shule kichwani, Eboue sasa ameanza kujuta kwa kutokuwa na ufahamu wa masuala ya kipesa. Alisema mara nyingi alizokuwa akienda benki alikuwa akiandamana na mkewe Aurelie. Mkewe sasa ndiye kila kitu. Mkewe anaonekana kama alimzidi ujanja katika baadhi ya mambo hasa ya kipesa.

Eboue anasimulia namna siku moja mtu wa benki alipomfuata mazoezini Arsenal na kumtaka asaini baadhi ya dokumenti, hakujua amesaini kitu gani na hapo lilianza tatizo. Eboue anataka wachezaji makinda wa Kiafrika kujifunza kupitia makosa yake.

“Mbaya sana, pesa zote nilizopata nilikuwa namtumia mke wangu na watoto wetu. Nilikuwa Uturuki nilipata Euro 8 milioni. Nilimtumia Euro 7 milioni nyumbani. Kila alichoniambia nisaini, nilisaini. Yeye ni mke wangu,” amesema.

Kwa sasa Eboue anapanda usafiri wa umma kwa sababu hata magari aliyokuwa akiyamiliki, sasa yanamilikiwa na mkewe. Kwenye hayo magari ya umma, Eboue amekuwa akijificha akiomba asifahamike kwa sababu bado yupo London.

Anasema anapomtazama mchezaji mwenzake wa zamani, Thierry Henry, akifanya uchambuzi kwenye televisheni, anajiona mjinga zaidi na kujichukia.

Kwa sasa, Eboue anategemea zaidi msaada wa dada yake, Yasmin, pamoja na staa wa zamani wa Portsmouth na Newcastle United, Lomana Lua Lua, ambao wamekuwa wakimsaidia katika baadhi ya mambo. Kwa watu hao ndiko Eboue ambako anakwenda kulala kwenye vibaraza vyao.

“Namshukuru bibi yangu kwa sababu alinifundisha kufua, kupika, kufagia na mengine mengi nilipokuwa mtoto. Hapa nilipo namshukuru tu Mungu kwa kuendelea kuwa hai, ukweli sipendi kabisa kilichotokea na sitaki kimtokee yeyote,” anasema.

Eboue anataka kurudi tena uwanjani kucheza.