Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Cheka, Miyeyusho aibu yao, aibu yetu

Bondia Francis Miyeyusho akiwa chini aamini macho yake baada ya kuangushwa na konde la mpinzani wake Sukkasen Kietyongyuth wa Thailand katika raundi ya kwanza ya pambano la raundi 10 uzito wa Feather  juzi Jumamosi Ukumbi wa PTA, Dar es Salaam. Miyeyusho hakuweza kusimama tena.

Muktasari:

  • Dalili za mabondia hao kufanya vibaya zilionekana tangu mwanzo baada ya Cheka kutoka sare na Gavad Zohrehvand wa Iran katika pambano la raundi nane uzito wa Light Heavy.

KISICHO riziki hakiliki. Mabondia wa Tanzania Francis Cheka ‘SMG’ na Francis Miyeyusho kwa pamoja wameshindwa kuipeperusha vyema bendera ya nchi katika mapambano yao ya kimataifa yaliyofanyika juzi Jumamosi usiku kwenye Ukumbi wa PTA, Dar es Salaam.

Dalili za mabondia hao kufanya vibaya zilionekana tangu mwanzo baada ya Cheka kutoka sare na Gavad Zohrehvand wa Iran katika pambano la raundi nane uzito wa Light Heavy.

Cheka alilalazimishwa kumaliza pambano hilo huku mpinzani wake akionekana kuwa hodari katika kukwepa na kupiga ngumi za kushtukiza na kumchanganya Cheka aliyeonekana kuchoka mapema.

Mwamuzi Anthony Luta alilazimika kuwapa somo la kutokushikana mabondia hao kwani walionekana kutaka kufikia mwisho wa raundi ya nane huku wakishindwa kuonyeshana ufundi zaidi.

Mara baada ya pambano hilo, Luta aliwanyanyua mikono juu Cheka na Gavad kuonyesha wametoka sare jambo lililozua miguno ukumbini hapo kwani mashabiki wengi walidhani Cheka amepigwa kwa pointi.

Jaji wa kwanza, Pembe Ndavu alitoa alama 76-76, wa pili Robert Kasigu alitoa alama 77-75 akimpa ushindi Gavad na wa mwisho, Rajab Mlowe alitoa alama 76-76, ndipo pambano hilo lilipoamuliwa kuwa sare.

Mkongwe wa ngumi nchini, Emmanuel Mlundwa alilifafanulia Mwanaspoti kuwa: “Majaji wawili wakitoa matokeo ya sare mmoja akitoa ushindi, matokeo yatakayokuwa na nguvu ni yale ya sare, hivyo majaji walikuwa sahihi kwa alama walizotoa.”

Akizungumza baada ya pambano hilo, Cheka alisema: “Ukweli nilichoka na katika ngumi lazima watu waelewe kuna matokeo matatu, kushinda, kutoka sare na kupigwa. Hili si jambo geni kwangu na kwa bondia yeyote yule.”

Gavad alisema: “Cheka ni bondia mzuri lakini anatakiwa kuongeza bidii ili aweze kufika mbali, namsifu ni mjanja na anavumilia ngumi akipigwa.”

Miyeyusho dah!

Pambano kubwa usiku wa juzi Jumamosi lilikuwa kati ya Miyeyusho na Sukkasen Kietyongyuth wa Thailand, ambalo nusura lisifanyike baada ya fedha za malipo ya Miyeyusho kutolipwa kwa wakati.

Ilichukua dakika 30 hadi Miyeyusho alipokubali kupanda ulingoni baada ya kulipwa Sh2 milioni zilizobaki katika malipo yake ya kucheza pambano hilo.

Mlezi wa ngumi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alilazimika kuingilia kati ili malipo hayo yafanyike na promota Mussa Kova wa Kampuni ya Mawenzi Production.

Baada ya Miyeyusho kukubali kupanda ulingoni, hakuweza kufua dafu na wakati nyimbo za taifa zinapigwa alionekana wazi kuwa na wasiwasi wa pambano hilo huku Kietyongyuth akionekana kujiamini zaidi.

Muda mfupi tu baada ya kengele kugongwa, Kietyongyuth alionekana kuwa makini na kumtandika makonde mfululizo Miyeyusho ambaye hakuonyesha jitihada zozote za kuzuia mashambulizi hayo na sekunde ya 30 alipigwa ngumi moja kali ya chembe iliyomyumbisha na kudondoka.

Mwamuzi Mlundwa alimuuliza Miyeyusho kuhusu kuendelea, naye akajibu ‘yes’, ndipo Kietyongyuth alipoendelea kumshambulia Miyeyusho na kumwangusha dakika 1 na sekunde 54 na kushindwa kuendelea, hivyo Kietyongyuth  akashinda kwa Knock Out ‘KO’.

Baada ya pambano hilo, Kamanda Kova aliliambia Mwanaspoti: “Kuna haja ya mabondia wetu kujiandaa kikamilifu, tazama kama hapa Miyeyusho alifikiria zaidi fedha kuliko mchezo na ndiyo maana amepoteza hakuwa makini na mchezo kabisa.”

Kabla ya mapambano hayo mawili, kulichezwa ngumi za utangulizi ambapo, Tasha Mjuaji alimshinda kwa pointi Steven Anastazi uzito wa Feather, Fabian Lyimo alimshinda Ramadhani Mnandi kwa pointi uzito wa Welter, Adam Yahya alimshinda kwa pointi Ramadhani Rajab uzito wa Light Fly na Sadik Momba alimshinda Epson John kwa pointi uzito wa Light, mapambano yote hayo yalikuwa ya raundi nne kila moja.

Ibrahim Class ‘Mawe’ alimshinda Mustafa Dotto kwa pointi pambano la raundi sita lisilo la ubingwa.