Chama amduwaza beki Horoya

Muktasari:

  • Fofana ambaye ni mrefu aliyekuwa katika ukuta wa Horoya wakati ikifumuliwa mabao 7-0 na Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku Chama akipiga hat-trick, aliliambia Mwanaspoti kama kuna mtu aliwavuruga katika mchezo huo basi ni kiungo huyo.

KIUNGO fundi wa mpira wa Simba, Clatous Chama yuko juu katika orodha ya wafungaji mabao wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi akiwa na manne sawa na Makabi Lilepo wa Al Hilal ya Sudan, huku beki wa Horoya Mohamed Fofana ametoa kauli ya kuumizwa na Mzambia huyo.

Fofana ambaye ni mrefu aliyekuwa katika ukuta wa Horoya wakati ikifumuliwa mabao 7-0 na Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku Chama akipiga hat-trick, aliliambia Mwanaspoti kama kuna mtu aliwavuruga katika mchezo huo basi ni kiungo huyo.

Beki huyo aliongeza kama kuna mtu anasema Chama hana kasi anamkosea, kwani jamaa alikuwa na athari kubwa kwake kwa mbio zake na hata utulivu wake akiwa na mpira.

"Nadhani yule aliyevaa jezi namba 17 (Chama) ni mchezaji hatari sana amesababisha matatizo makubwa sana kwenye eneo letu la ulinzi na hata katikati," alisema Fofana na kuongeza;

"Alikuwa na mbio ambazo tulishindwa kumdhibiti vizuri, lakini kitu kibaya zaidi ni utulivu wake anapokuwa na mpira, hana papara wala hachezi kwa presha kama wenzake, tumelazimika kukubali matokeo. Ukiangalia mabao yote aliyoyafunga utagundua utulivu wa akili yake, ameisaidia timu yake nafikiri kitu bora tumejifunza tutarudi kujipanga kwa mashindano yajayo."

Katika mchezo wa juzi dhidi ya Horoya, licha ya Chama kupiga hat-trick mabao mengine yaliwekwa kimiani na Sadio Kanoute na Jean Baleke.