Celtics ilivyotibua rekodi ya Mavericks

Muktasari:
- Ikiwa na faida ya kucheza nyumbani Celtics ilianza kwa ushindi wa vikapu 107-89 ikiwa ni tofauti ya pointi 18 dhidi ya Dallas.
FAINALI ya Ligi ya Mpira wa Kikapu Marekani (NBA) imeanza rasmi juzi Ijumaa kwenye Uwanja wa TD Garden, Boston, Ukanda wa Mashariki unaowakilishwa na Celtics na ilicheza dhidi ya Dallas Mavericks.
Ikiwa na faida ya kucheza nyumbani Celtics ilianza kwa ushindi wa vikapu 107-89 ikiwa ni tofauti ya pointi 18 dhidi ya Dallas.
Tofauti hiyo ni kama imetoa picha nzuri kwa Celtics na ina nafasi kubwa ya kutawala ‘series’ hii ya mechi nne au zaidi ya hizo kulingana na matokeo ya mechi zijazo huku kwa upande wa Dallas, ina kazi kubwa ya kufanya kwenye mechi tatu zijazo kuhakikisha inashinda ili kuongeza idadi ya mechi.
PORZINGS GUMZO
Katika mchezo huo wa kwanza wa fainali ya NBA, Gumzo lilikuwa ni kurejea wa nyota Kristaps Porzings Celtics, akitokea kwenye majeraha ya mguu, akikosekana kwa zaidi ya mechi 10 zilizopita za timu hiyo hususan zile za mtoano za Ukanda wa Mashariki.
Nyota huyo wa zamani wa Dallas, alikuwa sababu kubwa ya kuiangamiza timu yake aliyoichezea hivi karibuni kabla ya kuhamia Celtics, akifunga pointi 20 na ribaundi sita na kuivuruga kabisa Mavericks iliyojiandaa kuwakabili mastaa wawili zaidi, Jayson Tatum na Jaylen Brown.
USHINDI KWANZA, SASA NI NANE
Kama ilivyokuwa kwenye msimu mrefu, Celtics haijapoa kwenye kushinda mechi nyingi ndani ya mwaka huu na sasa imefikisha mechi nane mfululizo ilizoshinda hatua ya mtoano Mashariki na sasa kwenye fainali inakoweza kuongeza ikishinda mchezo ujao nyumbani kabla ya kuifuata Dallas kwao Uwanja wa American Airlines.
Celtics pia imeendeleza moto wake wa kutofungwa uwanja wake wa nyumbani katika kila mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano tangu ilipokipiga na Miami Heat hadi fainali ya ukanda dhidi ya Indiana Pacers na sasa fainali dhidi ya Dallas.
DALLAS WATIBUA REKODI YA UBINGWA
Mara ya mwisho Dallas kucheza fainali ya NBA, ni mwaka 2011 ikiongozwa na Dirk Nowitzki na mchezo wa kwanza wa ugenini ilishinda lakini safari hii rekodi hiyo imetibuliwa na Celtics, kinachoifanya iwe kwenye mtego wa kutoka nyuma na kushinda ubingwa baada ya miaka 13 kupita.
Dallas pia kabla ya kupoteza mchezo huu wa kwanza wa fainali ugenini, imetibua rekodi yao tamu ya kushinda mechi zote tano za ugenini ilizocheza kwenye fainali ya Ukanda wa Magharibi, lakini imeshindwa kuzuia kichapo mbele ya Celtics ambayo inasaka taji la 18 na la rekodi ya NBA kutoka mataji 17 iliyonayo sawa na Los Angeles Lakers.