CAF yampa mzuka Ouma Singida Black Stars

Muktasari:
- Timu hiyo imepata tiketi ya kushiriki michuano hiyo msimu ujao baada ya Yanga kuifunga JKT Tanzania mabao 2-0, katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), hivyo Singida Black Stars msimu huu kujihakikishia kumaliza ligi nafasi ya tatu au ya nne.
KOCHA wa Singida Black Stars raia wa Kenya, David Ouma amesema kitendo cha kupata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, kwao kama benchi la ufundi, viongozi na mashabiki ni jambo kubwa la kujivunia.
Timu hiyo imepata tiketi ya kushiriki michuano hiyo msimu ujao baada ya Yanga kuifunga JKT Tanzania mabao 2-0, katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), hivyo Singida Black Stars msimu huu kujihakikishia kumaliza ligi nafasi ya tatu au ya nne.
Iko hivi, kutokana na Tanzania kuwa na nafasi nne za uwakilishi wa michuano ya CAF, timu mbili za juu kwenye msimamo wa ligi huwa zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na inayomaliza nafasi ya tatu inacheza Kombe la Shirikisho sambamba na bingwa wa Kombe la FA.
Kitendo cha Yanga na Simba kujihakikishia kumaliza nafasi ya kwanza na ya pili katika Ligi Kuu na hata zikichukua ubingwa wa Kombe la FA msimu huu, zitacheza Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam FC na Singida zilizopo ya tatu na nne zitacheza Kombe la Shirikisho.
Akizungumzia hilo, Ouma alisema moja ya malengo yao waliyojiwekea msimu huu ni kumaliza nafasi nne za juu na kushiriki michuano ya Afrika msimu ujao, hivyo kwa hapa walipofikia wanajivunia kwa sababu kile walichokikusudia wamekitimiza.
“Tunashukuru sana kwa hapa tulipofikia kwa sababu haya ndio malengo yetu tangu mwanzoni mwa msimu, tunaendelea kujipanga na mechi mbili ngumu zijazo dhidi ya Simba, hivyo niseme wazi maandalizi kijumla yako vizuri hadi sasa,” alisema.
Ouma alisema wachezaji wote wamerejea kambini baada ya kutoa mapumziko ya siku nne na sasa wanajiandaa na mechi mbili mfululizo dhidi ya Simba za Ligi Kuu Bara itakayopigwa Mei 28, 2025 na ile ya nusu fainali ya Kombe la FA, Mei 31, 2025.
Ouma alianza kuiongoza timu hiyo Februari 4, 2025, baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Miloud Hamdi aliyetambulishwa Desemba 30, 2024, kuondoka kikosini na kutua Yanga anayoendelea kuifundisha.
Tangu Ouma akabidhiwe kikosi hicho kinachoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi na pointi 53, amekiongoza katika mechi 11 za Ligi Kuu Bara, kati ya hizo ameshinda sita, sare mbili na kupoteza tatu.