Burundi yaanza na ushindi CECAFA, yaichapa Uganda

Muktasari:
- Mashindano hayo yanayopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam yaliyoanza leo Juni 13 na kutamatika Juni 25.
TIMU ya taifa ya soka ya wanawake ya Burundi imeanza vyema kampeni za kutafuta ubingwa wa mashindano ya CECAFA Senior Women Championship 2025 kwa kuichapa Ugansa kwa bao 1-0.
Mashindano hayo yanayopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam yaliyoanza leo Juni 13 na kutamatika Juni 25.
Bao la Esperancia Habonemana dakika ya 75 lilifanya mchezo huo kwenda dakika 90 Burundi ikiongoza licha ya ubora pamoja na mashambulizi yaliyofanywa na Uganda.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Kocha wa Burundi, Niyungeko Alain Olivier amesema watakwenda kufanyia marekebisho baadhi ya maeneo hasa kwenye kutengeneza nafasi.
"Tumepata ushindi muhimu ambao unawapa motisha ya kupambana, tumecheza mechi ya kwanza na Uganda ni timu nzuri sana, " amesema kocha huyo na kuongeza;
"Uganda wamekuwa wakitufunga sana, lakini wachezaji wangu walijikaza na kama Uganda ingekuwa makini tungefungwa hata mabao mawili."
Kocha wa Uganda, Sheryl Botes amesema anajivunia namna timu ilivyocheza licha ya kupoteza mechi.
"Tunahitaji maandalizi ya kutosha, tunahitaji kupress mipira kwa sababu mechi hii tulikuwa nafasi ya kushinda kutokana na nafasi nyingi tulizotengeneza," amesema Sherly na kuongeza;
"Tunahitaji kushinda mechi zijazo na tunahitaji kufanya vizuri mechi zijazo na tutakwenda kwenye kiwanja cha mazoezi kurekebisha tuliyokosea."
Mechi nyingine inaendelea kwa sasa ikianza saa 1:00 usiku ni kati ya wenyeji Tanzania na Sudan Kusini uwanjani hapo.