Bosi ligi ya Rwanda avutiwa na uwekezaji Bara

Muktasari:
- Ligi Kuu Bara ni miongoni mwa ligi tano bora Afrika huku uwekezaji ambao umefanyika kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na klabu ukiifanya kuwa miongoni mwa zinazopedwa barani humu.
Mwenyekiti wa Ligi Kuu Rwanda ambaye pia ni mmiliki wa timu ya Gorilla ambayo inashiriki ligi hiyo, Mudaheranwa Hadji Yussuf amevutiwa na uwekezaji ambao umefanywa katika soka la Tanzania ambao unazifanya timu kufanya vizuri kimataifa.
Ligi Kuu Bara ni miongoni mwa ligi tano bora Afrika huku uwekezaji ambao umefanyika kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na klabu ukiifanya kuwa miongoni mwa zinazopedwa barani humu.
Hii ni kutokana na ushiriki wa timu za Yanga na Simba kimataifa ambazo zimekuwa na mwendelezo mzuri katika mashindano ya klabu Afrika.
Msimu huu 2024/25, timu mbili za Bara kati ya nne zilishiriki mashindano ya CAF zikitinga hatua ya makundi, ambapo Yanga iliyocheza Ligi ya Mabingwa na Simba Kombe la Shirikisho zilifika mbali, Simba ikitinga fainali huku Yanga ikifanya vizuri hatua ya makundi.
Msimu wa 2023/24 Yanga na Simba zote ziliishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, lakini 2022/23 Yanga ilifika fainali Kombe la Shirikisho huku Simba ikiishia robo fainali Shirikisho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mudaheranwa amesema wanatamani kuwa na uwekezaji mkubwa wa soka kama ilivyo Tanzania ambao utaifanya Rwanda kuwa bora kisoka Afrika.
"Tulikuja Tanzania kujifunza namna gani ambavyo wameweza kufanya haya yote ili na sisi tukafanye kule kwetu na soka letu liwe bora," amesema Mudaheranwa.
Ameongeza kuwa matarajio ni zaidi ya miaka miwili ijayo Rwanda kuwa na ligi bora ambayo itamvutia kila mchezaji kutoka pembe za Afrika kucheza kama ilivyo Bara.
Akizungumzia ushindani wa timu yake ya Gorilla katika ligi ya Rwanda kuhakikisha inaondoa ufalme wa Rayon na APR amesema ni mkubwa japo sio jambo la siku moja, lakini kutokana na uwekezaji ambao anaendeleaje kuufanya anaamini itanifikiwa kuwa miongoni mwa timu tishio na za kuogopwa nchini humo.
Mwenyekiti huyo pia amesema miongoni mwa vitu ambavyo vinavutia kwa sasa ni Uwanja wa Taifa wa Amahoro uliopo Kigali ambao umefanyiwa marekebisho makubwa na umekuwa kivutio kwa timu nyingi Afrika kwenda kucheza.