Bongo Zozo aahidi kuhamasisha utalii kwa wachezaji England kuja Tanzania

Muktasari:
Bongo Zozo aiahidi makubwa Tanzania, apania kuwahamasisha wachezaji wa timu za Uingereza kutembelea kwenye vivutio vya utalii
Dar es Salaam.Balozi mpya wa utalii Tanzania, Nick Reynald ‘Bongozozo’ ameahidi kutumia uwezo wake wote kuhamasisha wachezaji wa timu za Uingereza kuja kutalii nchini.
Bongo Zozo amesema mapenzi aliyonayo kwa Tanzania yanamfanya kuumiza kichwa ili kupata mawazo yatakayochangia kukuza sekta ya utalii na kuongeza idadi ya utalii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu lake hilo jipya.
Akizungumza leo baada ya kutangazwa rasmi na kukabidhiwa vitendea kazi na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bongo Zozo amesema atafanya ushawishi mkubwa kwenye michezo.
“Ninafahamiana na wachezaji wengi wa Uingereza na nina uwezo wa kuzifikia timu mbalimbali nitatumia uwezo wangu wote kuhakikisha wanaijua Tanzania na wanakuja kwenye vivutio. Haitaishia hapo watashindana wenyewe kwa wenyewe kuja hapa,”
“Juzi wakati wa mechi ya Aston Villa nilikuwa nawauliza mashabiki inaonekana hawaijui Tanzania sasa nitawapa fujo isiyoumiza wataijua tu na watakuja,”
Balozi huyo ameeleza kuwa serikali ya Tanzania imefanya uamuzi bora zaidi wa kumpa ubalozi kwani ataitumia nafasi hiyo kuonyesha mapenzi yake na nchi hiyo.
“Naipenda Tanzania, leo nimekataa kazi ambayo ingeningizia hela nyingi sana maana siku ninayotakiwa kuifanya nitakuwa na jukumu la kupeperusha bendera ya Tanzania kule Wembley sasa nimeona siwezi kuacha jukumu hilo,” amesema Bongo Zozo.