Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bila hata a.k.a miguu itazungumza tu!

Muktasari:

Sio mbaya sana kwa nyota wa soka nchini kuwa na majina ya utani maarufu kama a.k.a, kwani wakati mwingine huwasaidia kuwapa mzuka uwanjani kukiwasha kama wenye majina yao.

Dar es Salaam.Najua kuna baadhi yao hupachikwa majina ya utani na mashabiki wao. Ila wapo pia wanaojipa wenyewe a.k.a kwa kutaka kufananishwa na nyota wanaovutiwa nao kisoka (role model).

Sio mbaya sana kwa nyota wa soka nchini kuwa na majina ya utani maarufu kama a.k.a, kwani wakati mwingine huwasaidia kuwapa mzuka uwanjani kukiwasha kama wenye majina yao.

Hata miaka ya nyuma Tanzania ilikuwa na mastaa kibao waliojipa majina ya mastaa wakubwa duniani waliotamba enzi hizo. Wapo waliopachikwa kwa vile walikuwa wakisukuma gozi kama wakali hao waliotamba enzi hizo. Ndio maana haikuwa ajabu kusikia ama kuwaona nyota kibao wakiwa na a.k.a ya nyota wakali wa kimataifa wa zamani.

Sidhani kama majina ya kina Boi Idd 'Wikens', Rashid Idd 'Chama', Juma Pondamali 'Mensah' Mohammed Yahya 'Tostao', Razak Yusuf 'Careca' au Juma Amir Maftah 'Pele wa Mwanza' ni mageni kwa mashabiki wa soka wa kizazi hiki na kile cha nyuma.

Hata majina ya kina Said Mrisho 'Zico wa Kilosa', Twaha Hamidu 'Noriega', Steven Mapunda 'Garrincha', Frank Kasanga 'Bwalya' na mengineyo.

Ilivutia sana kusikia masikio wakati wakitangazwa na Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ama Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) katika matangazo ya mpira redioni.

Sio a.k.a hizo tu za nyota wa kigeni, nyota wa zamani pia walikuwa na majina ya utani ya vitu tofauti kulingana na mashabiki walivyowapachika ama wenyeji kujipa ndio maana tulikuwa na kina Sunday Manara 'Computer', akiwa ni mmoja ya nyota waliowahi kuibuka na kutamba nchini aliyekwa mahiri kwa kulisukuma gozi la ng'ombe na kuwa na akili ya haraka uwanjani kama kilivyo chombo hicho cha Kompyuta ambacho miaka hiyo hakikufahamika sana nchini.

Enzi hizo pia kulikuwa na watu kama Sanifu Lazaro 'Tingisha', aliyekuwa akiwatingisha kweli kweli mabeki kwa chenga zake uwanjani. Celestine 'Sikinde' Mbunga', Mohammed Kajole 'Machela', Salum Kabunda 'Ninja' aliyekuwa akikaba washambuliaji kininja kweli.

Yaani mguu wa mbavu, mguu wa shingo.

Tulikuwa na kina Abbas Dilunga 'Sungura' kwa ujanja wake uwanjani. Athuman Juma Chama 'Jogoo', Zamoyoni Mogella 'Golden Boy', Malota Soma 'Ball Juggler' ama John  Makelele 'Zig-Zag' ama Abeid Mziba 'Tekero', jina la mganga maarufu aliyevuma zamani. Mziba alikuwa Tekero kweli wa mipira ya vichwa. Kulikuwa na kina Makumbi Juma 'Homa ya Jiji', halafu Said Sued 'Scud' ni moja ya majina yaliyovuma japo straika huyo alivuma kwa msimu mmoja tu pale Jangwani mwaka 1991.

Straika huyo alibatizwa jina jilo kutokana na makombora yake yalivyowazima Wekundu wa Msimbazi nje ndani katika mechi ya watani mwaka huo wakati kukiwa na vita ya ghuba na Iraq chini ya Saddam Hussein ikitambia makombora yake ya Scud, huku Marekani ya George Bush mkubwa, ikiwa na Patroit.

Kifupi kulikuwa na a.k.a za kusisimua na zilizoendana na uhalisia wa wachezaji waliojipachika kwa mfano ulipokuwa ukisikia Bakar Malima 'Jembe Ulaya' ama Godwin Aswile 'Scania' au Willy Martin 'Gari Kubwa' ukienda uwanjani unakutana na watu wa shughuli kweli.

Mabeki hao walikuwa na miili jumba iliyowapa kazi kubwa washambuliaji kuwapenya uwanjani.

Ulipokuwa ukisikia Samli Ayoub 'Beki Mstaarabu' ama Method Mogella 'Fundi' au Ramadhani Lenny 'Maufi' a.k.a Mapafu ya Mbwa na Itutu Kiggy 'Road Master' ama Sunday Juma 'Pikipiki', hayakuwa majina tu bali ni uhalisia wa kile walichokuwa wakikonyesha uwanjani.

Hata katika zama hizi, kuna nyota kibao wana a.k.a za kusisimua, Ally Mustafa 'Barthez', Deo Munishi 'Dida', Hussein Sharrif 'Casillas', Haruna Moshi 'Boban', Ramadhan Chombo 'Redondo', Idd Seleman 'Ronaldo' Ramadhani Singano, Ibrahim Twaha na Abdallah Mguhi wenye a.k.a ya Messi, japo Singano alishalikataa jina hilo.

Pia kuna Andrew Vincent 'Dante', Abdallah Shaibu 'Ninja' na chipukizi wa Serengeti Boys', Kelvin John 'Mbappe' na kulikuwapo pia na Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Narejea tena sio mbaya wachezaji kuwa na a.k.a, lakini haya majina ya utani basi angalau yawe yanaendana na uhalisi wa kil wanachokionyesha nyota hao uwanjani. Nilikuwa nadhani ingekuwa bora nyota wa sasa wakaiacha miguu yao ikazungumza zaidi kuliko a.k.a zao.

Kwani nadhani hizi a.k.a kuna wakati zinawajaza ujinga. Majina haya ya utani yamekuwa makubwa kwao kuliko soka walilonalo mguuni ndio maana wanaonekana kituko.

Mashabiki wamekuwa wakiwapa majina makubwa na kusababisha walewe sifa na kuharibikiwa mapema kabla ya kutimiza ndoto zao.

Nakumbuka miaka kadhaa iliyopita niliwahi kumfanyia makala Singano kipindi kile ndio ameanza kuibuka ndani ya Simba akitokea timu ya Vijana U20, ambapo alikiri huwa analichukia sana jina la Messi. Nilimuuliza kwanini, naye alijibua ni kwa sababu anaamini hajafikia hata moja ya nane ya kile alichonacho Lionel Messi, huku akiwataka mashabiki wamuite majina yale halisi ya Ramadhani Singano. Singano alikuwa na sababu ya kulikataa jina la Messi.

Hata nyota wengine wajiangalia kama a.k.a wanazopewa zinaenda na uhalisi wa soka lao, kwani kuna wakati majina hayo ya utani unasababisha dharau kwao, hasa kama mchezaji anayejiita Ronaldo ama Neymar kisha uwanjani akawa anafanya madudu.

Ndivyo ukweli ulivyo, kuna makipa waliojibatiza ama kuitwa majina makubwa ya magolikipa wanaofunika Ulaya na duniani kwa ujumla, lakini uwanjani wanafungwa mabao ya ovyo kiasi cha kujidhalilisha na kuwadhalilisha wenye majina yao. Halafu mbona kuna wachezaji  kadhaa wanafanya vizuri na bado hawana a.k.a? Muangalieni Amissi Tambwe amekubali kuiacha miguu yake izungumze zaidi kuliko hata a.k.a, sawa tu na ilivyo kwa Emmanuel Okwi ama Eliud Ambokile. Ndio maana kiroho safi nasisitiza ni vyema zaidi wachezaji wa kizazi hiki wakajikita zaidi kusukuma gozi, kuliko kusaka a.k.a wasioweza kwenda nazo sambamba!

Hao kina Sunday Manara, Kitwana Manara 'Popat' ama Madaraka Seleman Mzee wa Kiminyio

walikuwa na a.k.a zilikuwa zikienda sambamba na walichokifanya uwanjani, pia hawakujipa

wenyewe bali walipachikwa na mashabiki kwa jinsi walivyowakuna kwa soka lao tamu!