Beki KMC mambo bado Al Hilal

Muktasari:
- Nyota huyo aliyeibuka Mchezaji Bora Chipukizi kwa msimu wa 2023-2024, alikuwa katika hatua za mwisho kumalizana na Al Hilal ya Sudan, lakini dili ni kama limebuma hivi.
BEKI wa pembeni wa KMC, Raheem Shomary aliyeripotiwa kupewa ruksa ya kwenda kujiunga na Al Hilal ya Sudan, amekiri mambo bado, kwani hakijaeleweka, ila anajipa moyo muda si mrefu kila kitu kitakaa sawa.
Nyota huyo aliyeibuka Mchezaji Bora Chipukizi kwa msimu wa 2023-2024, alikuwa katika hatua za mwisho kumalizana na Al Hilal ya Sudan, lakini dili ni kama limebuma hivi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Raheem alisema huenda huu sio wakati wa yeye kuitumikia timu hiyo akiamini muda sahihi wa kucheza soka la kulipwa nje utafika na ataondoka kama anavyoota kila siku.
Raheem alisema kwa sasa anazingatia kuipambania KMC kwa mechi mbili zilizosalia ili isishuke daraja, akisahau dili zima la Al Hilal kwamba mambo yamekuwa sivyo.
“Mimi mwenyewe nilikuwa nasikia tu mitandaoni, ila dili hilo lilikuwapo na viongozi wangu ndio walikuwa na mazungumzo na Hilal,” alisema Raheem na kuongeza;
“Msimu huu kwangu umekuwa mgumu sana kutokana na ushindani ulioonyeshwa na timu, unaona hadi sasa bado hajapatikana bingwa na kuna vita nyingine ya kushuka daraja kwa hiyo ni ngumu sana. Msimu uliopita timu ilimaliza nafasi ya tano lakini sasa tuko nafasi ya tisa bado tuna kazi ya kufanya kwenye mechi mbili zilizosalia, matamanio ni kushinda zote na kukusanya pointi sita.”
Beki huyo pamoja na wachezaji wanzie wanakabiliwa na mechi mbili za ugenini dhidi ya Mashujaa na Pamba Jiji zitakazopigwa kati ya Juni 18 na 22 kufunga msimu na Raheem alisema anaamini watafanya vyema na kuepuka kuangukia katika play-off ya kushuka daraja.
KMC iliyowahi kuiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2019, kwa sasa ipo nafasi ya tisa ikiwa na pointi 33 kupitia mechi 28.