Basigi: Mwendo ni huu hadi ubingwa

Muktasari:
- Simba inaongoza ligi hiyo baada ya klucheza mechi tisa ya duru la kwanza ikivuna pointi 25, ikishinda nane na sare moja, huku ikifunga mabao 27 na kuruhusu matano, inafuatiwa na JKT Queens yenye pointi 20.
BAADA ya kuhitimisha duru la kwanza Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) ikiwa kileleni bila kupoteza mchezo, kocha mkuu wa Simba Queens, Yussif Basigi amesema hawatabweteka na matokeo hayo kwani anakwenda kuwaongezea dozi vijana wake ili kuendeleza vipigo duru la pili ili kutetea ubingwa wa ligi hiyo.
Simba inaongoza ligi hiyo baada ya klucheza mechi tisa ya duru la kwanza ikivuna pointi 25, ikishinda nane na sare moja, huku ikifunga mabao 27 na kuruhusu matano, inafuatiwa na JKT Queens yenye pointi 20.
Watetezi hao walifunga mwaka 2024 kibabe juzi wakiichapa Alliance Girls kwa mabao 5-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kupitia mabao ya Jentrix Shikangwa aliyefunga mawili, Elizabeth Wambui, Precious Christopher na Esther Mayala.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Basigi raia wa Ghana alisema wachezaji wake wamefanya kazi kubwa mpaka sasa kwa kushinda mechi nane bila kupoteza mchezo, huku akisisitiza wanahitaji kuendelea na kasi hiyo ili mwisho wa msimu wawe mabingwa.
“Najua mzunguko wa pili utakuwa mgumu na wenye upinzani, lakini hatutazami nyuma tunahitaji kuongeza kasi ya mazoezi yetu kuendelea kuwa juu ya msimamo na mwisho wa msimu kuwa wa kwanza,” alisema Basigi.
Alisema katika mechi za nyuma safu yake ya ulinzi ilikuwa na udhaifu lakini sasa imerekebisha na kufanya vizuri ikiwa haijaruhusu bao katika mechi tatu mfululizo zilizopita, jambo wanalozidi kuimarisha.