Baobab, Aliance zashikilia ubingwa Simba, Yanga

JAPO leo Jumapili Mei 16, 2021 ni siku ya hitimisho la Ligi ya Wanawake Bara (WPL), Simba Queens yenye pointi 51 na Yanga Princess yenye pointi 50, zinasubiri dakika 90 kujua mmiliki halali wa taji hilo kwa msimu huu,.

Simba Queens ni wageni wa Baobab Queens mchezo utakaopigwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, wakati Yanga Princess itaikaribisha Alliance Girls kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam matokeo ya mechi hizo ndio yataamua bingwa. Mpishano wa pointi moja baina ya Simba Queens na Yanga Princess umegeuka mvuto kwa wadau wa soka na wengine kwenda mbali kwamba, laiti ingekuwa hivyo hadi kwenye timu za wanaume ingesaidia ushindani kuwa wa hali ya juu.

Aliyekuwa kocha wa Gwambina FC, Athuman Bilali ‘Bilo’ alisema kupishana pointi kunaleta mvuto kwenye mechi za mwisho kuwa na ushindani mkali, tofauti na timu ikiwa imejihakikishia ubingwa mapema.

“Sio Simba Queens wala Yanga Princess zote zina presha ya juu kwani hakuna mwenye uhakika wa kuwa salama katika mechi zao za mwisho,” alisema Bilo.

Straika wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel alisema soka la wanawake lina ushindani mkubwa na kupishana pointi moja kunaleta taswira nzuri ya kukuza vipaji. “Penye ushindani kuna kukua kwa vipaji vya wachezaji, imenifurahisha kuona sio Simba Queens wala Yanga Princess ambayo itakuwa na uhakika wa kuchukua ubingwa kabla ya mechi zao za mwisho,” alisema.


WASIKIE MAKOCHA

Kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema lengo lao ni kutetea taji baada ya kulichukua mwaka jana na kwamba, ushindani mkali ndio uliowatofautisha kwa pointi moja na Yanga Princess.

“Ligi ya msimu huu imekuwa bora zaidi, soka la wanawake linakua ndio maana tumetofautiana pointi moja na watani wetu wa jadi. Pamoja na hayo wachezaji wangu wana ari na nguvu ya kujitoa hadi tone la mwisho kuipa thamani timu kwa kuchukua ubingwa mara mbili mfululizo,” alisema.

Kocha wa Yanga Princess, Edna Lema alisema ligi ya msimu huu ilikuwa na ushindani wa juu ambao mechi za mwisho ndizo zitakazoamua nani bingwa, akitofautisha na uliopita ambao mechi tatu kabla alishajulikana nani anachukua taji hilo.

“Jambo la msingi nimewaandaa wachezaji wangu kushinda mechi dhidi ya Alliance Girls na kwamba lolote litakalotokea ni mapenzi ya Mungu endapo kama Simba Queens ikishinda huko Dodoma na huo ndio ushindani na mpira ulivyo,” alisema.

Wakati watani wakipigana vikumbo kuwania ubingwa, wapinzani wao nao wametamba kukomaa kwenye mechi hizo kwani Kocha wa Baobab Queens, Miraji Fundi amesema: “Wote tunahitaji ushindi hata kama hatubebi ubingwa, lakini itatusaidia kuongeza pointi, tumejipanga hivyo, niwaombe mashabiki kujitokeza kwa wingi katika mchezo huo.”

Kocha wa Alliance Girls, Ezekiel Chobanka alisema: “Tulianza na malengo ya ubingwa, baadaye ikaja kuwania nafasi nne za juu lakini vyote tumekosa, tunaenda kusaka heshima kukamilisha mashindano kwa ushindi japo wapinzani nao tunajua wamejiandaa, tutarajie mechi nzuri.”


ZILIZOSHUKA

Wakati bingwa anasakwa, kuna timu ambazo zinazoshuka ambazo ni ES Unyanyembe ambayo ilifutiwa matokeo kutokana na kushindwa kufika kwenye mechi na Mapinduzi Queens kabla ya jana Jumamosi ilikuwa imecheza mechi 20, ikatoka sare moja na kuchapwa mechi 19, hivyo ilimiliki pointi moja.


Imeandikwa na Olipa Assa, Clezencia Tryphone na Saddam Sadick