Bao la Haruna Niyonzima Kilomita 102 kwa saa

Muktasari:
Februari 27,2013, Niyonzima alifunga bao pekee la ushindi kwa Yanga dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kupiga shuti kali la kuzungusha akiwa nje ya eneo la hatari la wapinzani wao, umbali kama ule aliowafunga Gwambina FC.
MCHAMBUZI wa soka wa gazeti hili, Mwalimu Alex Kashasha amekadiria shuti la Haruna Niyonzima lililozaa bao pekee la ushindi la Yanga dhidi ya Gwambina FC juzi Jumatano katika Uwanja wa Uhuru kuwa lilikuwa na kasi ya Kilomita 102 kwa saa.
Mwalimu Kashasha ameliambia Mwanaspoti kuwa juhudi na ufundi binafsi wa Niyonzima kwa kiasi kikubwa ndio umemuwezesha kufunga bao hilo ambalo sio rahisi kufungwa na idadi kubwa ya wachezaji hapa nchini.
“Niyonzima alitumia akili sana kufunga bao lile kwa sababu kabla ya muda ule Yanga walikuwa wameshashambulia kwa mipira iliyokufa ‘set pieces’ nyingi lakini walishindwa kuzitumia.
Baada ya kupata mpira ule ambao ulikuwa umerudi baada ya kuokolewa (rebound), Niyonzima alikuwa anaelekea upande wa Mashariki ambako anacheza Bernard Morrison ambaye naye kiasili wanafanana kiuchezaji kwani wana kitu kinaitwa ‘ground skills management’.
Muda huo idadi kubwa ya mabeki wa Gwambina walisogea upande huo wa Mashariki na hawakudhani kama Niyonzima angeweza kubadili mawazo ndipo baada ya kugundua hilo, akaamua kwa haraka kufanya kitu kinaitwa ‘quick fast step’, akasogea kidogo na mpira na kupiga shuti la mbali (long range shoot) au ‘long range bullet’ ambalo likaenda kujaa nyavuni,” alisema Kashasha.
Mwalimu Kashasha alisema ingekuwa ni vigumu kipa wa Gwambina kuokoa shuti lile.
“Misingi (principles) ya ushambuliaji iko mitano na mojawapo ni ‘creativity’ (ubunifu), ambacho ndicho Niyonzima alikifanya.
Aligundua ingekuwa ni vigumu kwa mabeki kutibua kwa sababu ya ‘nature’ (asili) yake ya uchezaji lakini pia alikuwa katika ‘off angle’ (pembeni mwa usawa wa lango). Kwa hiyo kitendo kile ni muunganiko wa ‘natural reflexing’ (uamuzi wa haraka na sahihi) na pia ‘creativity’ (ubunifu)
Alikifanya katika upande wa kama mita 25 hivi kutoka langoni na shuti lile lilinyooka kwa nyuzi 180 na siku zote mashuti ya namna hiyo huwa ni magumu kwa kipa kuokoa. Unaweza kukadiria kasi ya shuti lile kama Kilomita 101 au 102 hivi kwa saa,” alisema Mwalimu Kashasha.
Mchambuzi huyo alisema ubunifu kama uliofanywa na Niyonzima ndio unahitajika kwa wachezaji wengi hapa Tanzania wawe nao kwa faida binafsi na timu zao.
Kashasha alisema ni mambo kama yale yanawezekana kwa kufanya mazoezi tu
“Bao lile lilikuja katika wakati mwafaka kutokana na mazingra ya ugumu wa mchezo ule ambao ulionekana ni vigumu kuwa na idadi kubwa ya mabao kwa sababu Yanga waliingia wakiwa na changamoto ya udhaifu wa safu yao ya ushambuliaji na Gwambina FC walikuwa wakicheza kwa nidhamu ya hali ya juu wakiamini wanacheza na timu kubwa na bora zaidi yao,” alisema mchambuzi huyo.
Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa Niyonzima kufunga mabao ambayo yamekuwa yakiacha gumzo na kuamua matokeo kwa Yanga kwani tayari ameshawahi kufanya hivyo hapo nyuma.
Februari 27,2013, Niyonzima alifunga bao pekee la ushindi kwa Yanga dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kupiga shuti kali la kuzungusha akiwa nje ya eneo la hatari la wapinzani wao, umbali kama ule aliowafunga Gwambina FC.
Kabla ya kufunga bao hilo dhidi ya Kagera Sugar, Niyonzima alipokea pasi ndefu ya nyuma kutoka kwa Kelvin Yondani akiwa upande wa kushoto na kumtoka beki mmoja wa Kagera kabla ya kuachia shuti hilo lililojaa wavuni.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Niyonzima tena aliifungia Yanga bao la ushindi dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Novemba 10, 2016 pindi walipoibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Akiwa nje ya eneo la hatari la Ruvu Shooting, Niyonzima alipokea pasi ya Donald Ngoma na kupiga shuti kali la mguu wa kulia ambalo lilikwenda moja kwa moja katika nyavu za wapinzani wao.