Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bando la Simba lachacha Kagera

Geofrey Taita wa Kagera Sugar akimdhibiti Ibrahim Ajib wa Simba wakati wa mchezo wao wa Ligi Kuu uliofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba jana. Kagera ilishinda kwa maao 2-0. Picha na Michael Jamson.

Muktasari:

Mabao mawili ya wachezaji wao wa zamani, Mbaraka Yusuf na Edward ‘Eddo’ Christopher katika kila kipindi cha mchezo huo uliokuwa mkali, yalitosha kuzima ndoto za Msimbazi kurejea kileleni kwani, imesaliwa na pointi zao 55 tu.

YANGA juzi Jumamosi ilipokuwa ikiinyuka Azam, mashabiki wa Simba waliofurika kwa wingi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam waliondoka uwanjani hapo huku wakisonya, lakini wakajipa moyo kuwa jana wangefanya yao mjini Bukoba.

Waliamini kuwa timu yao ingepata ushindi na kurejea kileleni mwa msimamo mbele ya Kagera Sugar, lakini kilichotokea baada ya dakika 90 kimewafanya waume meno kwa hasira baada ya kufumuliwa 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Mabao mawili ya wachezaji wao wa zamani, Mbaraka Yusuf na Edward ‘Eddo’ Christopher katika kila kipindi cha mchezo huo uliokuwa mkali, yalitosha kuzima ndoto za Msimbazi kurejea kileleni kwani, imesaliwa na pointi zao 55 tu.

Ikicheza mbele ya mabosi karibu wote wa Simba waliotua mjini Bukoba kwa ajili ya kuhakikisha chama lao linaanza harakati za kuvuna pointi tisa katika mechi zao tatu za Kanda ya Ziwa, Simba ilishindwa kabisa kufurukuta mbele ya Kagera.

Katika pambano hilo, lililosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka mkoani hapa, ilishuhudia Mbaraka Yusuf akifunga bao lake la 11 katika dakika ya 28 kwa kupiga shuti la ‘mwana ukome’ lililomuacha kipa Daniel Agyei, akiruka bila mafanikio.

Bao hilo lilidumu hadi mapumziko, kabla ya Eddo kuishtua Simba iliyowahi kumtema baada ya kumuibua kupitia timu ya vijana ya Simba B U20, baada ya kufunga bao la pili dakika chache tangu kuanza kwa kipindi cha pili.

Straika huyo, ambaye alianza kwa mara ya kwanza katika kikosi cha kwanza, alifunga bao hilo dakika ya 47 baada ya mabeki wa Simba kuzembea kuokoa mpira.

Simba ilitulia na kupanga mashambulizi yao kwa akili na dakika ya 61 kiungo Mzamiru Yasin aliifungia bao la kufutia machozi baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Kagera na yeye kufunga kiulaini likiwa bao lake la saba msimu huu.

Pamoja na kipigo, Simba inapaswa kujilaumui kutokana na kukosa mabao ya wazi hasa kipindi cha kwanza baada ya washambuliaji wake, Laudit Mavugo na Ibrahim Ajib kukosa umakini mbele ya lango la wenyeji ambao, ushindi huo umewafanya wapande hadi nafasi ya tatu na kuiengua Azam kwa tofauti ya pointi moja.

Kagera imefikisha pointi 45 baada ya mechi 25, pointi 10 nyuma dhidi ya Simba iliyosaliwa na pointi 55, huku Yanga ikiwa kileleni na alama zake 56.

Simba baada ya kupoteza pointi tatu za kwanza jana, sasa itakuwa na mtihani mwingine Jumatatu ijayo itakapokabiliana na Mbao kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza kabla ya kumalizana na Toto Africans Aprili 5 jijini humo.

Mabingwa hao wa zamani watalazimika kushinda ili kuweka hai matumaini yao ya kutwaa ubingwa ambao, iliunyakua mara ya mwisho msimu wa 2011-2012 na cha kufurahisha kwao ni kwamba, Yanga itakuwa na majukumu ya mechi zake za kimataifa dhidi ya MC Alger katika michezo ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo jana, African Lyon mapema mchana kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam iliichapa Stand United kwa bao 1-0, bao lilitupiwa kambani na Abdallah Mguhi dakika ya 45, huku Prisons na Mtibwa Sugar zikishindwa kufungana kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Majimaji Songea ikiwa uwanja wa nyumbani, ilipata ushindi mnono wa mbao 4-1 dhidi ya Toto Africans, huku Mwadui  na JKT Ruvu zikienda sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, mjini Shinyanga.