Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Baleke aizamisha tena Ihefu

Muktasari:

  • Straika Jean Baleke ndiye alikuwa shujaa wa mechi hiyo alipotupia mabao mawili ndani ya dakika mbili akianza 85 na 87 na kuwaacha Ihefu wakikosa la kufanya huku mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi wakipatwa mzuka.

Mfupa uliozishinda Yanga, Azam na Singida Big Stars umetafunwa kiulaini na Simba baada kuizamisha Ihefu mabao 2-0 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa uwanja wa Highland Estate wilayani Mbarali mkoani Mbeya.

Straika Jean Baleke ndiye alikuwa shujaa wa mechi hiyo alipotupia mabao mawili ndani ya dakika mbili akianza 85 na 87 na kuwaacha Ihefu wakikosa la kufanya huku mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi wakipatwa mzuka.
Baleke anafikisha mabao nane kwenye ligi kuu na 14 katika michezo yote aliyocheza akiitumikia Simba kwa mkopo akitokea TP Mazembe na kuendelea kuipa matumaini ya kuwania ubingwa msimu huu na watani zao Yanga wanaoongoza ligi kwa pointi 67.

Katika mchezo huo timu zote zilifanya mashambulizi lakini umakini ulikosekana kwa straika kuweza kumalizia mipira ya mwisho na kushuhudia kipindi cha kwanza kikimalizika kwa nguvu sawa ya bila kufungana.

Kabla ya dakika 45 za kwanza kocha mkuu wa Simba, Roberto Oliveria 'Robertinho' alimpumzisha Ismael Sawadogo na kumwingiza Nassoro Kapama baada ya nyota huyo kutomshawishi kocha huyo.

Kipindi cha pili Simba ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Habibu Kyombo na nafasi yake kuchukuliwa na John Bocco dakika ya 47 na kuwafanya Wekundu hao kuchangamka kupeleka mashambulizi langoni mwa Ihefu.

Hata hivyo Makipa wa timu zote Fikirini Bakari (Ihefu) na Ally Salim wa Simba walionesha kiwango kutokana na kuokoa hatari nyingi langoni mwao ambapo dakika ya 48 Adam Adam alioneshwa njano kabla ya kufanyiwa mabadiliko nafasi yake kuchukuliwa na Issah Ngoah,huku Mzamir Yassin naye akioneshwa kadi ya njano dakika ya 79.
Wachezaji Mzamir Yassin (Simba) na Yacouba Sogne wa Ihefu walionesha kiwango japokuwa nafasi walizopata hawakuweza kuzitumia vyema kabla ya Baleke kufanya maajabu dakika ya 85 na 87.

Simba wanabaki nafasi ya pili kwa pointi 60 baada ya mechi 25, huku Ihefu ikibaki nafasi ya sita kwa alama zao 30 baada ya michezo 26 na kubakiza minne kumaliza msimu huu.

Kocha Msaidizi wa Ihefu, Zuberi Katwila alisema walijipanga kushinda mchezo huo lakini walishindwa kutumia vyema nafasi walizopata na kwamba wanajiandaa na mechi ijayo.
"Tulijipanga na vijana walipambana lakini haikuwa bahati yetu na wapinzani wakatumia nafasi walizopata wakapata ushindi, tunaenda kurekebisha makosa yaliyoonekana katika mechi zijazo" alisema Katwila.

Kocha Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda alisema licha ya mashabiki kuonesha wasiwasi na kikosi kilichocheza lakini kila mmoja amesajiliwa kuitimikia timu na kwamba anawapongeza nyota wake kwa kazi nzuri.

"Kuwa na wasiwasi na kikosi lazima wajue kwamba hakuna ambaye ametoka nje ya timu, wachezaji wote wamesajiliwa kuitimikia timu hivyo matokeo haya ni mazuri kwetu na wametimiza wajibu, Ihefu wana timu imara tuliwaheshimu" alisema Mgunda.