Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Azizi KI kiwango cha maokoto

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Stephanie Aziz KI yuko kwenye moto kwa kiwango chake alioanza nao msimu huu na ni kama amezaliwa upya ndani ya jezi za njano na kijani tofauti kabisa na mwaka wake wa kwanza aliotua klabuni hapo.


MSIMU WA KICHOVU

Ukivuta picha presha ya usajili wa Aziz KI wakati anatua Yanga akitokea Asec Mimosas, kisha ukaangalia kiwango chake kilikuwa kinaleta wasiwasi mkubwa kikosini hapo.

Utakumbuka kuwa muda mwingi alikuwa akitokea benchi au wakati mwingine kutocheza kabisa huku akianza mechi chache zaidi. Wakati mwingine mashabiki wa timu hiyo walijikuta wakigawanyika kwa kushindwa kuelewa fomu yake ni ipi


FEI TOTO AMRUDISHA

Mwandishi wa makala haya aliwahi kufanya mahojiano na Aziz KI akamwambia kuwa ili awe bora uwanjani nafasi anayoipenda ni kucheza namba kumi yaani nyuma kidogo ya mshambuliaji wa mwisho. Akiwa hapo anaona anaweza kuonyesha kiwango bora na akathibitisha ubora wake.

Ni mara chache sana Aziz KI alikuwa akipewa nafasi ya kucheza eneo hilo kutokana na kocha wa wakati huo wa Yanga, Nasreddine Nabi kumuamini sana aliyekuwa kiungo wa timu hiyo Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Uwepo wa Fei Toto ulimfanya Nabi kumpa nafasi zaidi Mzanzibari huyo na kumpa ugumu Aziz KI kufanya makubwa kwenye eneo hilo, lakini Nabi alikuwa bado anatamani kumuona raia huyo wa Burkina Faso anapata nafasi - akijaribu kumbadilisha namba.

Nabi alikuwa wakati mwingine anampeleka Aziz KI kucheza pembeni akishambulia kutokea huko akicheza kwa mtindo wa nusu eneo, yaani anaibia kama winga, lakini pia kama namba kumi, ila bado hayakuonekana makali yake kwa kiasi kikubwa.

Baada ya utata wa kutaka kuondoka kwa Fei Toto, kulimfufua Aziz KI na kubaki mtawala pekee kwenye nafasi ya kucheza kama namba kumi. Akaanzia hapo kuuwasha moto ndani ya Yanga.


UKABAJI ULIMPONZA

Mfumo wa soka la Nabi ulikuwa unamtaka Aziz KI kama akicheza namba kumi, basi anashuka kuongeza idadi ya watu katikati ya uwanja kwa kukaba kidogo. Majukumu haya hayakuwa rafiki kwa kiungo huyo fundi na kujikuta anaingia katika utata na kocha wake huyo - majukumu ambayo hapo kabla yalikuwa rahisi kwa Fei Toto kuyatekeleza kwa kuwa kiungo huyo aliwahi kutumika kama kiungo mkabaji kabla ya kubadilishwa zaidi na kocha huyo.


MKALI WA MABAO

Hata kama Aziz KI hakucheza kwa kiwango kizuri katika mwaka wake wa kwanza, lakini kama kuna kitu ambacho kiungo huyo alijitofautisha na wengine na kujipa umuhimu, basi ni mabao yake muhimu ndani ya Yanga.

Alipiga bonge la bao akitokea benchi Yanga ikishinda katika ardhi ya Afrika Kaskazini kule Tunisia dhidi ya Club Africain - timu yake ikishinda kwa bao 1-0 kabla ya bao Yanga ilikuwa kwenye presha ya matokeo ikitoka kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Hilal. Ilirudi nchini ikakutana na Simba alikuwa yeye tena akiisawazishia timu bao muhimu la adhabu ndogo timu ikilazamisha sare muhimu dhidi ya watani wao.

Wakati Fei Toto akijiondoa Yanga wakiwa njiani kwenda kukutana na timu aliyotaka kuhamia, presha kubwa ilikuwa Yanga itafanya kipi huku mfungaji wa mabao mawili baina ya timu hizo akiwa amejiondoa?

Mfalme tena akawa Aziz KI akiifanya Yanga kutoka nyuma akifunga bao moja na kuhusika kutengeneza mengine mawili timu yake ikishinda mechi muhimu na ngumu kwa mabao 3-2, lakini yapo pia mabao mengine muhimu ya mashuti makali aliyofunga kwenye mechi zingine za ligi.


KAJIPATA KWA GAMONDI

Msimu huu Aziz KI chini ya kocha mpya Miguel Gamondi ni kama ameshamaliza harakati za kujityafuta sasa amejipata chini ya kocha huyo ambaye amemfanya kumuondolea zile pingu chini ya Nabi za kutakiwa kukaba sana badala yake amekuwa akimuacha muda mrefu kucheza huru.

Uhuru huo umekuwa mwiba kwa timu pinzani ambapo Yanga imekuwa na kasi kubwa inapoelekea lango la wapinzani, na mpishi mkubwa wa mabao amekuwa Aziz KI nyakati ambazo kila timu ambazo zinakwenda kukutana na mabingwa hao wanahofia  kukutana na kipigo cha mabao matano matano ambayo wamekuwa wakitoa karibuni.

Makali yake yamemfanya sasa kuwa sawa na kiungo mwenzake Maxi Nzengeli ambao kila mmoja ameshafunga mabao manne wakiwa wanaongoza kwa ufungaji kwenye mechi za mashindano walizocheza msimu huu huku Yanga ikiwa hatari sana eneo la kiungo.


MSIMU WA MAOKOTO

Mwisho wa msimu huu mkataba wa Aziz KI na Yanga utafikia tamati wakati ambao mashabiki wa Yanga wameshaanza kuvutiwa na mvinyo wake ambao ameendelea kuwakwekea kwenye glasi zao.

Hakuna namna kwa ubora alionao anayeweza kuthubutu kutamka kwamba fundi huyo wa mguu wa kushoto aondoke kama ambavyo waliondoka mastaa wengine Djuma Shaban au Mamadou Doumbia.

Utamu wa Aziz KI utakuwa shubiri mezani au kete muhimu atakapokutana na uongozi wa Yanga kujadili hatua ya kuurefusha mkataba wake.

Katika majadiliano hayo nyota huyo hatatumia nguvu kubwa kwani ataweka maneno kidogo kisha akiwaacha wakubwa  kufikiria kwa hesabu ndefu akijua tayari alishapanda mbegu sahihi kwa kiwango chake anachoendelea kuonyesha hivi sasa.

Acha tuone mambo yatakavyokwenda nani atamshika mwenzake pale kwenye kochi jeupe ghorofani.