Azam yawapoteza Simba, Yanga

Muktasari:
- Azam imeonekana kuwa na mwelekeo mzuri zaidi kwa kushinda michezo minne ambayo ni dhidi ya Namungo (1-0), Tanzania Prisons (2-0), KenGold (4-1) na Yanga (1-0) kisha kutoka suluhu dhidi ya Mashujaa (0-0), na kuifanya kuwa timu pekee katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi ambayo haijapoteza mchezo kwenye michezo mitano iliyopita.
NDANI ya michezo mitano iliyopita ya Ligi Kuu Bara, Azam FC imeonekana kuwa kwenye kiwango bora zaidi mbele ya wakongwe Simba na Yanga kwa kukusanya pointi nyingi (13).
Azam imeonekana kuwa na mwelekeo mzuri zaidi kwa kushinda michezo minne ambayo ni dhidi ya Namungo (1-0), Tanzania Prisons (2-0), KenGold (4-1) na Yanga (1-0) kisha kutoka suluhu dhidi ya Mashujaa (0-0), na kuifanya kuwa timu pekee katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi ambayo haijapoteza mchezo kwenye michezo mitano iliyopita.
Vijana hao wa Kocha Rachid Taoussi, wamefunga mabao manane na kuruhusu moja, ikimaanisha kuwa safu yao ya ulinzi imeimarika na pia uwezo wa kushambulia umeongezeka.
Pointi 13 walizokusanya Azam zinaashiria kuwa timu hiyo ipo katika mwelekeo mzuri katika kurudi kwenye ushindani wa ubingwa ikiwa imeachwa pointi nne na vinara Simba wenye 25.
“Bado tuna kazi kubwa na ngumu ya kufanya mbele yetu, tunatakiwa kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi katika michezo ijayo ili kuendelea kusogea nafasi za juu,” alisema Rachid ambaye kikosi chake kipo nafasi ya nne katika msimamo wa ligi na pointi 21.
Simba ambayo inaongoza ligi kwa sasa, katika mechi tano za mwisho kabla ya ligi kusimama imejikusanyia pointi 12, ikishinda michezo minne ambayo ni dhidi ya Tanzania Prisons (1-0), Namungo (3-0), Mashujaa (1-0), KMC (4-0) na kupoteza mmoja dhidi ya Yanga kwa bao 1-0, huku ikifunga mabao 9 na kuruhusu moja. Simba pia imeonyesha uimara kwenye safu ya ulinzi kama Azam.
Hata hivyo licha ya Simba kuzidiwa kete na Azam kwa kuangalia fomu ya timu hizo kwa michezo mitano iliyopita, wekundu wa Msimbazi wao ndio vinara wa Ligi Kuu Bara wakiongoza kwa pointi 25.
Singida Black Stars wako katika nafasi ya tatu ambapo mechi tano za mwisho wamekusanya pointi 10 baada ya kushinda michezo mitatu, sare mmoja na kupoteza mmoja. Wana idadi ndogo ya mabao ya kufunga (5) ikilinganishwa na Azam na Simba, ufanisi wao katika ulinzi umewabeba kwa kuruhusu bao moja.
Nafasi yao ya tatu inaonyesha kuwa bado wanajipambania lakini watapaswa kuimarisha safu ya ushambuliaji ili kuwa washindani wenye nguvu kwa timu za juu zaidi.
“Tunatakiwa kuonyesha mabadiliko baada ya mapumziko ya kalenda ya FIFA, tutakuwa na mechi ngumu ambazo tutatakiwa kucheza ndani ya kipindi kifupi,” alisema Kocha wa Singida Black Stars, Patrick Aussems.
Yanga SC, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, wamekuwa na kipindi kigumu kwenye michezo mitano iliyopita. Wakiwa wamekusanya pointi 9 kutokana na ushindi wa michezo mitatu na kupoteza miwili mfululizo dhidi ya Azam (1-0) na Tabora United (3-1), Yanga ambao wapo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 24, wanahitaji kuboresha matokeo yao ligi ikirejea.
Ndani ya michezo hiyo mitano, Yanga wamefunga mabao matano na kuruhusu manne, jambo linaloashiria kuwa safu yao ya ushambuliaji na ulinzi zinahitaji mabadiliko ili kuwa imara zaidi.
Ndani ya michezo mitano iliyopita, Namungo ya Juma Mgunda ndio timu ambayo hali yake inaonekana kuwa tete zaidi kwani imekusanya pointi tatu zilizotokana na kushinda mchezo mmoja dhidi ya Pamba (1-0), huku ikipoteza mara nne dhidi ya Azam (1-0), Singida Black Stars (2-0), Simba (3-0), KMC (1-0).
Akizungumzia matokeo hayo, Mgunda alisema: “Hali sio nzuri, lazima tuamke! Tumepoteza michezo mingi jambo ambalo halileti picha nzuri. Tumekuwa tukifanya mazoezi, lakini tunahitaji kuonyesha mabadiliko makubwa uwanjani.”
Mgunda aliongeza kuwa kikosi chake kinahitaji uwajibikaji zaidi kutoka kwa kila mchezaji, huku akisisitiza umuhimu wa kurejea kwenye wimbi la ushindi kama njia pekee ya kuwaweka salama.
“Tutafanya mabadiliko ya mbinu na kuangalia baadhi ya nafasi ambazo zimekuwa na mapungufu, lengo ni kuhakikisha tunapata matokeo mazuri. Ligi bado ni ndefu, lakini hatuwezi kuendelea kupoteza kwa kiwango hiki,” alieleza Mgunda.
Namungo sasa inakabiliwa na kibarua kigumu kuhakikisha inarejea kwenye mwenendo mzuri, ikitarajia kurekebisha makosa yao ili waweze kujiimarisha na kushindana vilivyo na timu zinazoshika nafasi za juu.
Hivyo Mgunda anakibarua cha kuhakikisha kikosi hicho chenye maskani yake kusini mwa Tanzania kinarejea kwenye wimbi la matokeo mazuri ambalo walikuwa nalo msimu uliopita.