Azam, Yanga zakwama nyumbani

Timu za Yanga na Azam za Tanzania zimeshindwa kufika fainali ya Kombe la Kagame licha ya kuwa wenyeji wa mashindano hayo yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Mabingwa mara tano wa kombe hilo, Yanga katika mashindano ya msimu huu walitolewa mapema kwenye hatua ya makundi baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi A lililoongozwa na Express ya Uganda, Nyasa Big Bullets ya Malawi, Yanga na Atlabara ya Sudan Kusini.
Azam wao ambao ni mabingwa mara mbili wa kombe hilo walitolewa juzi kwenye mchezo wa nusu fainali na Nyassa Big Bullets kwa mikwaju ya penati 4-2, baada ya dakika 120 za mechi hiyo kumalizika wa sare ya mabao 2-2.

Azam ikiwa imebeba matumaini ya Watanzania wengi kwenye mashindano hayo msimu huu baada ya Yanga kutolewa, katika mchezo wa nusu fainali iliingia na wachezaji wale wale vijana waliocheza mechi za awali.
Dakika ya pili tu ya mchezo huo Azam waliiruhusu Nyasa kupata bao la kwanza lililofungwa na Bright Munthaly, bao lililodumu hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika.
Kipindi cha pili kilirejea kwa Azam kuongeza kasi na dakika ya 67, mshambuliaji Paul Peter aliisawazishia Azam na dakika ya 73 Oscar Masai aliifungia Azam bao la pili na la kuongoza kabla ya Nyasa kusawazisha dakika ya 78 na dakika 90 kumalizika kwa mabao 2-2.
Baada ya hapo ziliongezwa dakika 30 ambazo hazikuzaa matunda kwa timu zote mbili na kufanya ipigwe mikwaju ya Penalti na Nyasa kushinda kwa kufunga 4-2, na kutinga fainali.