Azam isivyotaka utani 2021/22

Beki wa kushoto, Edward Manyama
DIRISHA la usajili linatarajiwa kufungwa mwishoni mwa mwezi huu, na sasa kila timu inafanya usajili kuimarisha kikosi kutokana na upungufu ulioonekana msimu ulioisha.
Matajiri wa Dar es Salaam, Azam FC wameshafanya usajili wa nyota saba baada ya kutangaza kuwaacha watano ambao ni Obrey Chirwa, Yacob Mohammed, Ally Niyonzima, Monzinzi Mpina na Never Tegere.
Kwa maana hiyo, ujio wa wakali saba utasababisha vita kubwa ya namba. Wapya watakutana na wale waliokuwepo msimu uliopita waliofanya vizuri na kujihakikisha namba. Patachimbika.
Makala haya yanachambua nyota hao watakavyokuwa na kazi ngumu kumshawishi kocha George Lwandamina ili wajihakikishie namba kikosi cha kwanza.
EDWARD MANYAMA
Uwezo wake mkubwa akiwa Namungo alikocheza msimu mmoja na kutimkia Ruvu Shooting ulizivutia Simba, Yanga na Azam zilizoonyesha kuhitaji saini yake.
Hata hivyo, washambuliaji wa timu pinzani walipata tabu kupita ngome ya timu alizocheza beki namba tatu na alifanya vyema zaidi Namungo akiwa miongoni walioiwakilisha kwenye Kombe la Shirikisho Afrika. Ubora wake uliwafanya viongozi wa Azam kumwaga mamillion na kufanikiwa kunasa saini yake.
Hivyo, ili kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, inabidi Manyama aonyeshe uwezo mkubwa mazoezini kumshawishi Lwandamina amwamini maana anaenda kukutana na kisiki, Bruce Kangwa, ambaye amekuwa akiaminiwa tangu amesajiliwa kikosini hapo.
PAUL KATEMA
Katema ambaye ni kiungo mkabaji amesajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Red Arrows ya Zambia na anaungana na Charles Zuru na Rodgers Kola wote kutoka taifa moja. Usajili wake unatarajiwa kutoa changamoto kwa wazawa wanaocheza nafasi hiyo ambao wameaminiwa zaidi ya misimu miwili.

Kiungo mkabaji wa kimataifa wa Zambia, Paul Katema
Tangu Azam imepanda daraja imekuwa ikitoa nafasi kwa wazawa kucheza nafasi ya kiungo tofauti na nafasi nyingine ambazo wamekuwa wakichanganya na wageni, lakini msimu ujao moto utawaka safu ya kiungo kutokana na ongezeko la nyota wa kigeni.
CHARLES ZURU
Mzambia huyu anatarajiwa kukipiga Azam msimu ujao baada ya kusajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili akitokea klabu ya Cape Town City ya Afrika Kusini..
Ili aweze kucheza atakuwa na vita mbili eneo la kiungo mkabaji na Frank Domayo na Mudathil Yahya ambao wamekuwa wakibadilishana kucheza kikosi cha kwanza.
KENETH MGUNA
Huyu anatokea Kenya alikokuwa chaguo la kwanza Gor Mahia, lakini akiwa Azam atakuwa na kazi ngumu kusaka namba mbele ya Abubakar Salum ‘Sure Boy’ ambaye amecheza kwa muda mrefu ndani ya timu hiyo.
Ubora wa Sure Boy katika kutengeneza mashambulizi na kutibua mipango ya wapinzani wao eneo la kati kila mmoja analitambua na amekuwa akipiga mashuti ya mbali na kufunga, hiyo ni moja ya changamoto kwa Muguna
IDRISA MBOMBO
Mshambuliaji wa kimataifa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Idris Mbombo amesajiliwa na Azam FC kwa mkataba wa miaka miwili akitokea El Gounah ya Misri.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Idris Mbombo
Mshambuliaji huyo hatari aliyewahi kuzichezea kwa mafanikio timu za Nkana, Zesco United na Kabwe Warriors zote za Zambia, anakuja kuongeza nguvu safu ya ushambuliaji ambayo msimu uliopita ilimtegemea zaidi Mzimbabwe Prince Dube.
Upinzani utakuwa mkali kutokana na uwepo wa Dube na Ayub Lyanga, na atakayeonyesha uwezo ndiye atapata nafasi ya kucheza, kwani Lwandamina ameonekana kupenda kutumia straika mmoja asilia katika kila mechi.
RODGERS KOLA
Ni ongezeko la mshambuliaji mwingine ndani ya Azam. hHii ni baada ya kuachwa kwa Chirwa sasa wanaunda utatu wa Dube, Kola na Mbombo. Azam wamefanikisha usajili wa nyota huyo kwa mkataba wa miaka miwili.
Kola anayecheza nafasi ya ushambuliaji atakumbana na upinzani wa namba kutoka kwa Idd Seleman ‘Nado’ na ili kuweza kuikamatia nafasi kikosi cha kwanza itabidi aonyeshe uwezo wake mbele ya washambuliaji hao wazoefu walioibeba timu msimu ulioisha na kuisaidia kumaliza ya tatu ikipata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
AHMED SULEIMAN
Amejiunga na Azam kwa lengo la kuziba nafasi iliyoachwa na David Kisu ambaye amemaliza mkataba na timu hiyo, pia kuongeza ushindani kwa kipa namba moja Mganda, Mathias Kigonya.
Kipa huyo mwenye umbo kubwa amesaini mkataba wa miaka miwili na kuwaacha KMKM waliokuwa wakimtegemea sambamba na timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, amesajiliwa ili kuongeza nguvu katika eneo kipa.
MANYAMA, MUGUNA
Manyama anasema hajakurupuka kutua Azam na kuweka wazi kuwa hajutii kuwa miongoni mwa watakaovaa uzi wa timu hiyo msimu ujao.
“Kuhusu changamoto ya namba najiamini na kabla ya kusaini nilijua naenda kukutana na nani, hivyo naweza kusema nimepima na kuona nitacheza, naomba sapoti tu kutoka kwa wenzangu ili tuweze kufikia mafanikio,” anasema.
Naye Muguna anasema: “Naweza kucheza nafasi zote kasoro kipa, hivyo nina nafasi kubwa ya kupata nafasi ya kucheza kama mwalimu atanielewa kwenye mazoezi. Mpira mbali na kipaji kuna maelekezo kutoka kwa mwalimu, hivyo nikipewa majukumu nitafanya kama inavyotakiwa.”
WADAU WAZUNGUMZA
Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula anasema msimu ujao Azam itaiwakilisha nchi kimataifa na kwa usajili wanaoendelea kufanya anaamini utaleta ushindani ndani na nje na kuipa thamani ligi ya Bongo.
“Wachezaji wengi waliowasajili wana uzoefu, hivyo tunategemea mambo mazuri ndani na kimataifa wamesajili washambuliaji wazuri, pia tunategemea mabao mengi,” anasema.
Kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ anasema Azam wanatakiwa kuwafuatilia vya kutosha wachezaji wao wote wapya ambao watawasajili msimu huu, kwani haipendeza kulingana na ubora wa timu yao kusajili wachezaji wenye viwango vya kupanda na kushuka.
“Kama wachezaji hao wanaotajwa Azam imewapata, maana yake watakuwa wameimarisha timu yao na kwenda kufanya vizuri katika mashindano yote msimu ujao, lakini kama wakifanya makosa hapo wanaweza kujikuta na timu ya kawaida.”