Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rekodi nne Yanga ilivyobeba Ubingwa

REKODI Pict

YANGA imetetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba, katika mechi ya Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Juni 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.


Mechi hiyo ya mwisho ya ligi msimu huu, iliamua bingwa wa Ligi Kuu kutokana na tofauti ya gepu la pointi moja kabla ya kukutanana  Yanga ilihitaji sare au ushindi tu kwa sababu ilikuwa inaongoza na pointi 79, ikifuatiwa na Simba iliyokuwa na pointi 78.


Katika mechi hiyo, Pacome Zouzoua aliifungia Yanga bao la kwanza kwa penalti ya dakika ya 66 baada ya nyota huyo kufanyiwa madhambi eneo la hatari na kipa wa Simba, Moussa Camara, huku Clement Mzize akifunga la pili dakika ya 86.

Yanga imemaliza msimu na pointi 82, ikishinda mechi 27, sare moja na kupoteza miwili kati ya 30 iliyocheza, ikitwaa taji la 31, la Ligi Kuu tangu mwaka 1965, huku Simba ikiwa ya pili na pointi 78, ikishinda 25, sare tatu na kupoteza miwili. 


BAO LA KWANZA KWA MZIZE

Bao la Mzize dakika ya 86, lilikuwa ni la 14 kwenye Ligi Kuu Bara kwake msimu huu, ingawa ni la kwanza kufunga katika mechi ya Dabi ya Kariakoo, tangu aanze kukitumikia kikosi hicho msimu wa 2022-2023. 

Katika msimu wake wa kwanza yaani 2022-2023, nyota huyo alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu, pia alichangia upatikanaji wa mabao sita, akifunga matano na kuasisti moja kati ya 61 ya timu nzima.

Msimu huo, Yanga ilifika hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kukosa ubingwa kwa faida ya bao la ugenini mbele ya USM Alger ya Algeria baada ya sare ya jumla ya mabao 2-2, ikichapwa nyumbani 2-1, kisha ugenini ikashinda 1-0.

Msimu wake wa pili 2023-2024, Mzize alichangia mabao 13, baada ya kufunga sita na kuasisti saba kati ya 71 ya kikosi hicho kizima, kilichotwaa tena ubingwa wa Ligi Kuu Bara ukiwa ni wa tatu mfululizo kutokana na kukusanya pointi zake 80.

Katika misimu mitatu, huu ndio bora zaidi kwa mshambuliaji huyo kwa sababu amechangia mabao 19, ya Ligi Kuu Bara kati ya 83, yaliyofungwa na kikosi hicho kizima kilichomaliza na pointi 82, baada ya kufunga mabao 14 na kuasisti matano.

PILA 01

HAMDI AKUMBUSHIA YA OMOG

Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi ameandika rekodi nyingine mpya ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho, huku akiingia katikati ya msimu akifuata pia nyayo za aliyekuwa Kocha wa Azam FC raia wa Cameroon, Joseph Marius Omog.

Hamdi mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa huku akiwa na leseni A ya UEFA, alitua nchini kujiunga na Singida Black Stars, Desemba 30, 2024, ingawa hakuiongoza mechi yoyote hadi Yanga ilipoinasa saini yake rasmi, Februari 4, 2025.

Kocha huyo alitambulishwa Yanga baada ya kuondoka kwa Mjerumani, Sead Ramovic aliyejiuzulu mwenyewe, Februari 4, 2025, kwa makubaliano ya pande mbili, tangu atambulishwe kikosini humo Novemba 15, 2024, akitokea TS Galaxy ya Afrika Kusini.

Baada ya kuondoka Ramovic aliyejiunga na CR Belouizdad ya Algeria, ndipo Hamdi akakiongoza kikosi hicho na kukipa taji la nne mfululizo la Ligi Kuu Bara na la 31, kwa jumla tangu mwaka 1965, akiwa ameingia katikati ya msimu huu.

Katika Ligi Kuu Bara, mechi hiyo na Simba ilikuwa ya 13 kwa Hamdi kuiongoza Yanga tangu alipoanza kibarua hicho Februari 4, 2025 na ameshinda 12 na kutoka suluhu mmoja tu ambao ilikuwa ya kwanza dhidi ya JKT Tanzania, Februari 10, 2025.

Mechi hiyo ya suluhu (0-0) dhidi ya maafande wa JKT Tanzania iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar, ndiyo iliyokuwa ya kwanza kwa kocha huyo, japo kuanzia hapo ameshinda zote 12, mfululizo hadi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

Sasa kitendo cha Hamdi kutwaa ubingwa huo, kinakumbushia msimu wa 2013-2014, ambao Azam FC ilitwaa pia taji la Ligi Kuu na ilianza msimu na Kocha raia wa England, Stewart Hall, kisha kuondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Joseph Omog.

Hall alitua Azam FC msimu wa 2010-2012, ingawa aliondoka Novemba 7, 2013, baada tu ya mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza msimu wa 2013-2014, dhidi ya Mbeya City, iliyofanyika Azam Complex na kuisha sare ya mabao 3-3.

Kitendo cha kuondoka Hall, viongozi wa Azam FC wakavamia AC Leopards ya DR Congo na kumchukua Omog aliyetoka kuipa taji la Kombe la Shirikisho Afrika na kumalizia msimu huo na kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Azam FC kama alivyofanya Hamdi.

PILA 02

REKODI YA SIMBA YAVUNJWA

Kitendo cha Simba kupoteza pambano hilo kwa mabao 2-0, sio kuendeleza tu unyonge kwa Yanga katika Ligi Kuu Bara, kwani pia rekodi ya timu hiyo ya kucheza mechi nyingi bila ya kupoteza imevunjwa, tangu mara ya mwisho ilipochapwa, Oktoba 19, 2024.

Tangu Simba ilipochapwa bao 1-0, dhidi ya Yanga, Oktoba 19, 2024, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kikosi hicho kilikuwa kimecheza jumla ya mechi 23 bila ya kupoteza na kati ya hizo kilishinda 21, huku miwili iliyobaki ikimalizika kwa sare. 

Kitendo cha Yanga kushinda tena, kimeifanya kuivurugia Simba kwani tangu pambano hilo la Oktoba 19, 2024, liliipa nguvu ya kucheza mechi 23 bila ya kupoteza, kabla ya rekodi hiyo kuja kutibuliwa Juni 25, 2025, ilipokubali kuchapwa mabao 2-0.

PILA 03

YANGA YARUDIA REKODI YA 2016-2017

Kitendo cha Yanga kutwaa ubingwa msimu huu katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara, kimeifanya timu hiyo kurudia rekodi iliyoiweka pia ya msimu wa 2016-2017, iliponyakua ubingwa huo baada ya ushindani mkubwa uliokuwepo kati yake na Simba.

Katika msimu huo wa 2016-2017, Yanga ilimaliza kinara na pointi 68, baada ya kucheza mechi 30, ikishinda 21, sare tano na kupoteza minne, ikiwa ni idadi sawa kwa kila kitu na Simba iliyomaliza ya pili, japo zilitofautiana kwa mabao tu.

Msimu huo, timu hizo zilishinda mechi 21, sare tano na kupoteza minne, ingawa Yanga ilifunga mabao 57 na kuruhusu 14, huku kwa upande wa Simba ikifunga mabao 50 na kuruhusu 17, hivyo kutofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Katika mechi za mwishoni zilizoamua bingwa msimu huo, Yanga ilihitimisha msimu huo kwa kuifunga Tanzania Prisons mabao 2-0, Mei 6, 2017, huku kwa upande wa Simba iliyocheza raundi ya 30, Mei 7, 2017, iliifunga African Lyon pia mabao 2-1.

PILA 04

MSIKIE HAMDI

Baada ya mechi hiyo, Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi anasema imekuwa furaha kubwa kwake kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho kwa mara ya kwanza, huku akiwapongeza viongozi na mashabiki kwa sapoti waliyompatia tangu mwanzo.

“Kwangu ni heshima kubwa sana lakini hizi zote ziende kwa wachezaji kwa kutambua malengo ya timu yalikuwa ni nini kiasi cha kufanikisha hili, bado tuna taji moja lililobaki ambalo pia tunahitaji kuchukua ili tumalize vizuri msimu,” anasema.