Asukile atoa matumaini Tanzania Prisons

Muktasari:
- Kwa sasa timu hiyo ipo nafasi ya 13 na pointi 30, imebakiwa na mechi mbili dhidi ya Yanga, Juni 18 mwaka huu (nyumbani) kisha kumalizia msimu ugenini Juni 22 mwaka huu kukipiga na Singida Black Stars.
STAA wa zamani wa Tanzania Prisons, Benjamin Asukile amesema pamoja na presha iliyopo kukwepa kushuka daraja, lakini upo uwezekano wa kubaki salama Ligi Kuu kwa timu hiyo msimu ujao.
Kwa sasa timu hiyo ipo nafasi ya 13 na pointi 30, imebakiwa na mechi mbili dhidi ya Yanga, Juni 18 mwaka huu (nyumbani) kisha kumalizia msimu ugenini Juni 22 mwaka huu kukipiga na Singida Black Stars.
Maafande hao wapo katika hesabu nzito dhidi ya timu nyingine nane kwenye vita ya kukwepa kucheza play off ya kubaki baada ya KenGold na Kagera Sugar kushuka daraja moja kwa moja.
Timu hizo ni JKT Tanzania iliyopo nafasi ya sita na pointi 35, Dodoma Jiji (pointi 34), Mashujaa (pointi 33) sawa na KMC, Coastal Union (pointi 31) sawa na Namungo, Pamba Jiji (pointi 30) na Fountain Gate (pointi 29).
Asukile ambaye kwa sasa yupo kwenye benchi la ufundi la Tanzania Prisons, alisema baada ya kufanikiwa kuepuka kushuka daraja moja kwa moja, nguvu na akili yao ni kuona namna ya kuzicheza mechi mbili ili kubaki salama zaidi. Alisema ubora walioonyesha wachezaji ndani ya uwanja hadi sasa ni wa kupongezwa kwani ligi imekuwa ngumu ndio maana vita hadi sasa ni kali akiwaomba kuendelea kupambana.
“Kwanza tunashukuru kuwa salama hadi sasa, vijana wamepambana, bado kazi ni ngumu ila tukikaza tutabaki Ligi Kuu, hizi mechi mbili ni kufia uwanjani kupata pointi sita,” alisema Asukile.