Ashanti wamtaka Juma Kaseja bure

Juma Kaseja akiwajibika mazoezini
Muktasari:
Katika michezo minne waliyocheza Ashanti United wamepoteza mitatu na kutoka sare mmoja huku wakiendelea kuburuza mkiani katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.
ASHANTI United imemwambia aliyekuwa kipa namba moja wa Simba, Juma Kaseja: “Jitolee kucheza Ashanti kama Said Maulid ‘SMG’ ujenge heshima ya kuendelea kuitumikia timu ya Taifa lako na mashabiki wako.”
Katika michezo minne waliyocheza Ashanti United wamepoteza mitatu na kutoka sare mmoja huku wakiendelea kuburuza mkiani katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Timu hiyo inatamani kumsajili Juma Kaseja ingawa wanamshindwa kutokana na kutaka dau kubwa la Sh50 milioni.
Fununu za kumtaka kipa huyo zilichukua nafasi baada ya Kaseja kuonekana akifanya mazoezi na kikosi hicho katika uwanja wao wa Msimbazi lakini ukweli wa mambo umewekwa wazi na Katibu Mkuu wa Ashanti, Aboubakar Silas kwamba hawamuwezi.
“Ni kweli Kaseja amekubali kujiunga na sisi lakini tunafahamu hatuna uwezo wa kumlipa hata kidogo, tunajikuna mahali mkono unapofikia hatuwezi kumsajili mchezaji mmoja kwa bei kubwa wakati timu ina hali mbaya ya kifedha, kama anaweza ajitolee kama Said Maulid,” alisema.