Arsenal mikononi mwa Demba Ba

Wachezaji wa Arsenal wakiwa kwenye mazoezi
Muktasari:
Celtic iliyokuwa imechapwa mabao 6-1 na Legia Warsaw imepangwa kumenyana na mabingwa wa Slovenia, Maribor baada ya Waskochi hao kupeta kufuatia Legia kuchezesha mchezaji asiyeruhusiwa.
ARSENAL imepangwa kuivaa Besiktas ya Uturuki inayochezewa na straika wa zamani wa Chelsea, Demba Ba katika mechi za mchujo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya upangaji wa ratiba hiyo iliyofanyika mjini Nyon, Uswisi jana Ijumaa.
Celtic iliyokuwa imechapwa mabao 6-1 na Legia Warsaw imepangwa kumenyana na mabingwa wa Slovenia, Maribor baada ya Waskochi hao kupeta kufuatia Legia kuchezesha mchezaji asiyeruhusiwa.
Arsenal itakuwa na shughuli pevu ugenini kwa Besiktas ambayo mashambulizi yake yataongozwa na Ba, aliyejiunga nao mwezi uliopita akitokea Stamford Bridge. Ba anawafahamu vizuri Arsenal baada ya kumenyana nao mara kadhaa kwenye Ligi Kuu England alipokuwa kwenye kikosi cha Newcastle United na baadaye Chelsea.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Arsenal kukutana na timu za Uturuki kwenye hatua hiyo baada ya mwaka jana kuwafunga Fenerbahce mabao 5-0. Mechi za kwanza zitafanyika kati ya Agosti 19 na Agosti 20 na marudiano ni wiki moja baadaye.