Amunike kuinoa Serengeti Boys

Muktasari:
- Kidao alisema itarejea Dar es Salaam Februari 27 na Machi Mosi itaondoka kwenda Uturuki.
Dar es Salaam. Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike amejumuishwa kwenye benchi la ufundi la timu ya vijana (Serengeti Boys) inayojiandaa na fainali za Afrika za vijana (Afcon U17).
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao alisema Amunike yuko mkoani Arusha ilipo timu hiyo inayonolewa na kocha mkuu, Oscar Mirambo.
"Timu yetu inaendelea vizuri na kambi mkoani Arusha na tayari kocha wa Amunike na Ninje (Ammy ambaye ni Mkurugenzi wa ufundi wa TFF) wako kule kwa ajili kuongeza nguvu kwenye timu ya taifa ya Serengeti," alisema Kidao.
Kidao alitoa kauli hiyo mbele ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kwenye kikao cha tisa cha maandalizi ya Afcon ya vijana ambayo Tanzania itakuwa mwenyeji baadae Aprili.
Alisema Kocha Amunike na Ninje wameteua vijana 60 katika mikoa ya Mwanza, Morogoro, Tanga, Kagera na Zanzibar kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye timu hiyo ya vijana.
"Katika vijana hao, 10 au 20 watajumuishwa kwenye timu yetu ya Serengeti ambayo itakwenda Uturuki kwenye mashindano ya UEFA lakini pia itaweka kambi huko kujiandaa na AFCON," alisema Kidao.
Alisema vijana hao wataungana na wengine 20 kati ya 30 walioko kwenye timu hiyo ambao watakwenda Uturuki.
"Tumeamua kuongeza wachezaji wengine kama tahadhari ili itakapofikia wanahitajika kupima kipimo cha MRI basi tuwe na kikosi kipana," alisema.
Akizungumzia ratiba ya timu hiyo, Kidao alisema itarejea Dar es Salaam Februari 27 na Machi Mosi itaondoka kwenda Uturuki.
"Wakiwa kule watacheza pia mechi tano za kirafiki na watarejea nchini Machi 24 na siku inayofuata wataondoka kwenda Rwanda kwenye mashindano maalumu hadi Aprili 5 watakaporejea nchini tayari kwa Afcon," alisema.
S:Serengeti Boys itafungua dimba dhidi ya Nigeria kwenye fainali hizo zitakazofanyika jijini Dar es Salaam.