Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ally J afunguka Mzee Yusuf kuhusishwa ajali ya Five -Stars

Muktasari:

Ally Juma Nassib ‘Ally J’, ambaye alinusurika katika ajali hiyo, anaendelea kupata machungu ya ajali ile, akisema ni ngumu kufutika akilini mwake japo kwa sasa anaendelea na maisha yake baada ya ajali.

MEDANI ya muziki Tanzania na nchi nzima kwa ujumla vilitikisika kufuatia ajali ya gari ya kutisha iliyoua wanamuziki 13 wa Kundi la Taarabu la Five Stars mwaka 2011.

Simanzi ilitawala nchi, wasanii walilia, wadau wa burudani waliingia baridi na vyombo vya habari nchi nzima vilitawaliwa na ripoti kuhusu tukio hilo kubwa la kugusa mioyo ya watu.

Miaka takriban minane sasa, Tanzania imeshaugulia na kusahau machungu, lakini hali ni tofauti kwa mtu ambaye alikuwamo ndani ya gari aina ya Toyota Coaster lililochukua roho za wenzake 13 akishuhudia.

Ally Juma Nassib ‘Ally J’, ambaye alinusurika katika ajali hiyo, anaendelea kupata machungu ya ajali ile, akisema ni ngumu kufutika akilini mwake japo kwa sasa anaendelea na maisha yake baada ya ajali.

Achinja mbuzi

Ally Jay anasema daima anawaombea wenzake waliotangulia mbele za haki, ila baada ya kunusurika katika ajali hiyo hakuwa na hali nzuri alikuwa ni kama mtu aliyechanganyikiwa kiakili, hivyo alichinja mbuzi na kusomewa dua na amekuwa sawa hadi sasa.

“Unajua hii iko wazi kwa baadhi ya watu kutokana na imani zao, kuwa wakipata matukio kama haya na siyo matukio tu, hata mtu ukitaka kufanya dua ili mambo yako yaende, huwa watu wanachinja mnyama. Na mimi nilivyobahatika kutoka mzima katika ile ajali, nilifanya dua na kuchinja mbuzi. Nilienda kwa marehemu Sheikh Zuberi Jangwani kwenda kupata dua na hali ikatulia kama hivi unavyoniona,” anasema Ally J.

Anasema kupona kwake katika tukio hilo ni miujiza kwani alitoka kwenye ajali bila ya kuwa hata na mchubuko mwilini ilhali wenzake 13 walifariki dunia.

“Baada ya kishindo cha ajali nilijikuta niko chini. Nilijikongoja na nikaweza kuitambua miili ya wenzangu kwa kuimulika kwa tochi. Ilikuwa inatisha kwakweli. Ilikuwa ngumu kuamini watu uliokuwa unacheka nao dakika chache zilizopita sasa ni marehemu,” anasimulia.

“Pale kwenye tukio, nilipata nguvu ya ajabu hadi kufikia hatua ya kutafuta miili ya wenzangu kwa tochi na kufanikisha zoezi la kuipeleka hospitali.

“Lakini baada ya hapo ndiyo sikuwa sawa kabisa kiakili. Nilikuwa kama nimechanganyikiwa. Ilinisumbua sana.

“Ni kweli binadamu tumeumbiwa kusahau, lakini katika hili mimi hapana aisee.”

Kuhusiwa Mzee Yusuf?

Baada ya ajali hiyo, maneno mengi yalizuka mtaani ya kuhusisha ajali hiyo na mambo ya kishirikina na madai hayo yalimuangukia Alhaji Mzee Yusuf kutokana na kipindi hicho alikuwa akimiliki Kundi la Jahazi Modern Taraabu na wasanii wake kama watano akiwemo dada yake, Khadija Yusuf waliondoka katika bendi yake na kuanzisha Five Stars iliyokuwa inakuja juu na kutishia bendi nyingine za taarabu.

Ila kwa madai hayo Ally J anasema habari hizo alizisikia ila kwa upande wake yeye hana uhakika nazo kwani anachojua yeye ajali imetokana kwa mapenzi ya Mungu.

“Hizo habari za Mzee Yusuf kudaiwa kuwa ndiye alifanya mambo ya kishirikina hadi ajali hiyo kutokea nimezisikia tu kwa watu, ila siwezi kuthibitisha, sina uhakika nalo kwani nina imani kila kitu kinapangwa na Mungu, kama jambo la mwanadamu huwezi sikia hivyo ila kama yupo aliyesababisha basi Mungu atamuhukumu yeye.”

Kwa sasa yuko wapi?

Ally J kwa sasa anapiga kinanda katika The Kilimanjaro Band ‘Wana Njenje’ baada ya kutoka Jahazi Morden Taarabu.

“Unajua kabla sijajiunga na Njenje mwaka 2017 Mzee Yusuf alipoachana na bendi yake ya Jahazi viongozi wa bendi hiyo walinifuata nikafanye nao kazi, si kama ilikuwa mara ya kwanza kufanya nao kazi, huko nyuma Mzee alipokuwepo kwenye bendi nilishawahi kufanya kazi naye kwenye bendi hiyo.

“Sasa baada ya kujiengua kwa Mzee Jahazi tulifanikiwa kutengeneza nyimbo mbili, ‘Jicho la Mungu’ aliouimba Mosi Sulemani na ‘Nataka Jibu’ alioimba Mwasiti Kitoronto.

“Hapo ikaja sintomfahamu ndani ya bendi. Vitu vingi nilikuwa nafanya kama najitolea tu nikiamini kuna siku tukizindua tunaweza kupata pesa. Mara pesa ikaja. Nilipoona ninaejitolea sipatiwi kitu nikaamua kuachana na hiyo bendi,” anasema.

Ally J anasema akaamua kuandika katika mtandao wa Instagram kuwa yuko huru, hivyo anayetaka kufanya kazi naye waonane wafanye maelewano, ndipo alipotokea mpiga tumba wa Njenje, Abuu Mwichumu akamuunganisha na Waziri Ally wakampa programu ya mazoezi yao ya bendi na ndiyo hadi leo yupo hapo.

Historia yake ya muziki

Ally J alianza muziki mwaka 1997 akiwa Shule ya Msingi Lumumba, ambapo alikuwa akienda kwenye bendi ya muziki wa taarabu ya Alwatan. Mwalimu wake wa kwanza ni Haidary na ndiye aliyemfundisha kupiga kinanda.

Mwaka 2004 alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Bendi ya Bembea Taarabu iliyokuwa na makazi yake Magomeni Mapipa akiwa na marehemu Nasma Khamis Kidogo, Hussein Kibao na wengine wengi.

“Baada ya hapo mwaka 2005 kulianzishwa Zanzibar Stars ambayo ilikuja kutamba na Albamu ya ‘Tutabanana Hapahapa’. Siku ya uzinduzi wa albamu hiyo waliichukua bendi ya Bembea kuwasindikiza. Uzinduzi ulipoisha Mzee Yusuf, Zubeda Mlamali na Feruz Juma wakanishawishi nijiunge na Zanzibar Stars, nikakubali. Nikiwa nao nikapiga kinanda katika albamu nne ikiwamo ya ‘Nimekinai Umaskini Wangu’,” anasema.

Ilipofika mwaka 2007 Ally J alihamia East African Melody akijumuika na kina Mwanaidi Shaabani, Khadija Yusuf, Hassan Soud na wengine ambapo hapa walitoa albamu inayoitwa ‘Uso wa Guzo’ yeye akipiga kinanda.

Ally J anasema hakukaa sana Melody, aliondoka na kwenda Oman na baadhi ya wanamuziki wa bendi ya Stono Musica waliogawanyika kipindi hicho. Alikuwa na Patcho Mwamba, Malu Stonch na wengine na aliendelea kupiga kazi Oman kwa muda mrefu.

Anasema kisha Mzee Yusuf akafanya mawasiliano naye na kumwambia arudi kwani anataka kuanzisha Bendi ya Jahazi.

Ally J anasema aliporudi hakujiunga na Jahazi bali alichukuliwa na Zanzibar Stars na kutoa Albamu ya ‘Raha ya Mapenzi’ na ‘Rindima Rindima’ zilizoimbwa marehemu Mariam Khamisi.

Mwaka 2008 akajiunga Jahazi na kurekodi Albamu ya ‘V.I.P’ wimbo huo uliimbwa na MzeeYusuf na hapo Ally J anasema ndipo alipoanza kufahamika zaidi. Mwaka 2009 ndipo likaja sakata la kuanzisha Bendi ya Five Stars chini ya Selemani Jitu.