Alliance FC yazifuata Simba, Yanga kusajili wachezaji wa nje

Muktasari:
- Alliance ambao wanatarajia kushiriki Ligi Kuu msimu ujao kwa mara ya kwanza,juzi ilianza matizi kwenye uwanja wa CCM Kirumba chini ya Benchi la Ufundi likiongozwa Kocha Mnyarwanda Kayiranga Jean Baptiste.
Mwanza. Mambo yameanza kuiva Mwanza, wakati Mbao ikitoka kumtangaza Kocha mpya Amri Said, jirani zao Alliance wameshusha silaha nne mpya kutoka Rwanda na Uganda.
Alliance ambao wanatarajia kushiriki Ligi Kuu msimu ujao kwa mara ya kwanza,juzi ilianza matizi kwenye uwanja wa CCM Kirumba chini ya Benchi la Ufundi likiongozwa Kocha Mnyarwanda Kayiranga Jean Baptiste.
Timu hiyo iliyopanda daraja kucheza msimu unaofuata wa Ligi Kuu, imeanza kufuata nyayo za timu vigo kama Simba na Yanga ambazo zimekuwa na utamaduni wa kusajili nyota kutoka Rwanda na Uganda.
Nyota hao ambao gazeti hili liliwashuhudia wakijifua katika mazoezi yao maalumu ikiwa ni kuwaangalia uwezo wao kama wataweza kufiti katika Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Wakali hao ni pamoja na Washambuliaji, Karekezi Jean aliyewahi kukipiga timu za Poster Rangers na St.George ya Ethiopia na Gidion Sekamwa wa Villa Sports ya Uganda.
Wengine ni Beki wa Kati, Frank Kawoya aliyetoka Klabu ya Polisi Uganda na Kiungo Sentamu Frank wa Express ya Uganda ambao wote hao juzi walianza mazoezi.
Kocha Msaidizi wa Klabu hiyo,Kessy Mziray alisema kuwa nyota hao wapo kwenye majaribio kuona kama watafuzu kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu.
Alisema kuwa baada ya siku chache watatoa ripoti kwa uongozi juu ya kiwango cha wachezaji hao na kama wataridhika basi watavaa uzi na kuanza kazi.
“Ndio tumeanza mazoezi kuangalia uwezo wao, bahati nzuri benchi la ufundi wote tupo kwahiyo tutaangalia kama watafuzu basi tutatoa ripoti kwa uongozi,” alisema Mziray.
Kocha huyo aliongeza kuwa timu hiyo bado inapokea wachezaji wanaojiamini kuwa na uwezo kujitokeza katika majaribio ambayo yatadumu kwa siku 14.