AJ hoi tena akimkosa Fury

Muktasari:
Linakua pambano la pili kwa Joshua kupoteza na kuvuliwa mikanda yake minne ya uzito wa juu Duniani (Heavyweight).
POINTI za majaji wote watatu (Unanimous Decision) waliompatia ushindi bondia Oleksandr Usyk, zimemvua mataji yote manne ya uzito wa juu Duniani, bondia Anthony Joshua.
Joshua ambaye alikuwa nyumbani, kwenye dimba la soka la Tottenham Hotspur pale London Kaskazini, alikumbana na kichapo cha mapema kabisa kutoka kwa mpinzani wake Oleksandr Usyk aliyeshinda kwa 117-112, 116-112 na 115-113 baada ya kumaliza vema kwenye raundi zote 12 za pambano hilo lililokua gumu kwa wote wawili.
Mwanzo mzuri alioanza nao Usyk kwenye raundi za awali, ndizo zilichangia kwa kiasi kikubwa kumpa ushindi huo usiotarajiwa, licha ya Joshua kujaribu kutafuta Knockout 'KO' mwishoni bila mafanikio.
Msako wa 'KO' kwa Joshua kwenye raundi za mwisho, ni kama alikumbuka shuka alfajiri baada ya kugundua pambano linaelekea kumalizika na mpinzani wake aliandikisha pointi nyingi zaidi yake, haikushangaza pale Usyk alipotangazwa kama mshindi baada ya kufanikiwa kumaliza raundi zote 12.
Ushindi huo usio na shaka kwa Usyk, zimempatia umwamba bondia huyo kutoka Ukraine, ambaye sasa amemvua Joshua mikanda yote minne ya WBO, IBF, IBO na Super WBA aliyokua nayo baada ya mara ya mwisho kuwapiga mabondia Andy Ruiz Jr na Kubrat Pulev.
Usyk pia amefuta ndoto za Joshua na promota wake Eddie Hearn kuendelea na mipango ya kupigana dhidi ya bondia Tyson Fury, ambao walishakubaliana na promota wake Bob Arum kupigana mwezi Agosti mwaka huu.
Wakati Tyson Fury akitarajiwa kupigana pambano la tatu dhidi ya Deontay Wilder mnamo Oktoba 09, kuwania mkanda wa WBC, itamlazimu kusubiri hatma ya Joshua kwa Usyk.
Joshua 'AJ' ana kila sababu ya kumshukuru promota wake Hearn, ambaye aliweka kipengele cha kurudiana (rematch) kati yake na Usyk wakati wa kusaini mkataba wa pambano hilo.
Hii inamaanisha kwamba, Joshua ana nafasi ya kujipanga upya kurudisha mikanda yake minne dhidi ya Usyk kwenye pambano namba mbili, ndipo ajue nini hatma ya pambano lake dhidi ya Fury ambaye naye anatakiwa kumshinda tena Wilder mwezi ujao.