Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fadlu aweka kila kitu wazi atakavyoikabili Berkane

Muktasari:

  • Akizungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar, Fadlu amesema: “Ndiyo, tulikuwa tumejiandaa kikamilifu kwa mechi ya kwanza. Tulikuwa tumepanga kila kitu kiufundi na kimkakati, lakini jambo kubwa zaidi lilikuwa kuwapa wachezaji uzoefu wa dakika zile 20 za mwanzo kwa sababu unaweza kuwa na mpango mzuri lakini hali halisi ya uwanja na mazingira ya fainali huwezi kuifundisha darasani. Lazima waishi nayo, wapitie, na wakue kupitia hilo.”

KOCHA  wa Simba SC, Fadlu Davids, amesema kikosi kiko tayari kwa mechi ya fainali ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane huku akisisitiza kuwa wachezaji wameshajifunza kupitia maumivu ya dakika 20 za kwanza kule Morocco.

Akizungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar, Fadlu amesema: “Ndiyo, tulikuwa tumejiandaa kikamilifu kwa mechi ya kwanza. Tulikuwa tumepanga kila kitu kiufundi na kimkakati, lakini jambo kubwa zaidi lilikuwa kuwapa wachezaji uzoefu wa dakika zile 20 za mwanzo kwa sababu unaweza kuwa na mpango mzuri lakini hali halisi ya uwanja na mazingira ya fainali huwezi kuifundisha darasani. Lazima waishi nayo, wapitie, na wakue kupitia hilo.”

Katika mechi wa kwanza iliyochezwa wikiendi iliyopita nchini Morocco, Simba ilikubali kichapo cha mabao 2-0. Hata hivyo, Fadlu anaamini wapo tayari kwa pambano la marudiano, licha ya mchezo huo kuhamishiwa Zanzibar badala ya Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

“Tunajua Benjamin Mkapa ni faida kubwa kwetu. Ni uwanja wenye historia. Timu nyingi kubwa kama Al Ahly na Wydad zimekuja pale na kutoka bila pointi. Lakini hatutaficha, tunaumia kwamba mechi hii haipo pale,” amesema Fadlu na kuongeza.

“Lakini hata hivyo, hatutumii hilo kama kisingizio. Tumekuja hapa Zanzibar tukiwa na imani na fahari. Tunaamini Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla watasimama nyuma yetu.”

Fadlu amesema ana uhakika kuwa wakati basi la timu likifika uwanjani, wataona mashabiki wao wakilizunguka, wakipiga kelele na kushangilia kama ilivyo kawaida yao Simba, jambo analoamini litatoa msukumo kwa wachezaji kupambana hadi mwisho.

“Tunahitaji kuigeuza Zanzibar kuwa nyumbani kwetu. Tuifanye iwe kama Benjamin Mkapa. Hilo linawezekana kama Watanzania wataungana na kusimama pamoja nasi. Huu ni wakati wa umoja.”

Akizungumzia mechi ya kwanza, Fadlu amesema pamoja na kufungwa, walijifunza mengi.

“Nilipata kadi ya njano si kwa sababu ya hasira bali kuamsha wachezaji wangu. Walihitaji kujua kwamba hii ni vita, na licha ya mazingira magumu, wao ni timu nzuri na wanaweza kushindana.

“Berkane walikuwa na mabao mawili, lakini kwa takwimu walikuwa na makadirio ya kufunga bao 1.18, Camara (Mussa) alifanya kazi kubwa sana, aliokoa bao la wazi, hilo lilitufanya tubaki mchezoni,” amesema Fadlu na kuongeza.

“Tulikuwa na nafasi nusu-nusu, wao pia, lakini mwisho wa siku, wachezaji wangu walitoka uwanjani wakiwa na imani kuwa wanaweza kushindana. Tumejifunza, tumejipanga, na sasa tunasubiri mchezo wa marudiano kwa matumaini makubwa.”

Simba inahitaji ushindi wa mabao matatu bila nyavu zao kuguswa kutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza. Mechi hiyo ya marudiano inatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.