Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Coastal yatoa msimamo wa Lawi

Lawi Pict

Muktasari:

  • Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Omary Ayoub amesema kwa sasa wako tayari kukaa mezani kujadili mauzo ya Lawi.

COASTAL Union imeweka wazi msimamo wake juu ya beki wa klabu hiyo, Lameck Lawi ambaye kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa kutakiwa na timu za Simba na Yanga.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Omary Ayoub amesema kwa sasa wako tayari kukaa mezani kujadili mauzo ya Lawi.

Ikumbukwe kuwa kabla ya msimu kuanza, Coastal Union iliingia kwenye mgogoro na Simba kuhusu beki huyo ambaye alitakiwa kutua kwa Wekundu hao.

Lawi ambaye msimu uliopita alifanya vizuri na kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Ligi Kuu Bara, kiwango hicho kiliwavutia mabosi wa Simba na kutangaza kumsajili kabla ya Coastal kuibuka na kupinga usajili huo, ikabaki na mchezaji wake.

Akizungumza na Mwanaspoti, bosi huyo wa Coastal Union alisema kwa sasa wako tayari kukaa chini na timu yoyote itakayomtaka mchezaji huyo huku akibainisha kwamba hakuna timu iliyogonga hodi kutaka saini ya Lawi, akiitaja Simba pia haijarudi.

“Lawi ni mchezaji wa gharama sana, hivyo timu zinazokuja kumtaka zijipange kisawasawa, kwani bado ana mkataba wa muda mrefu,” alisema bosi huyo huku akigoma kuweka wazi mkataba huo ni mrefu kiasi gani ingawa Mwanaspoti linafahamu kwamba Lawi mkataba wake na Coastal Union unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu na hivi karibuni ilipanga kukutana naye kwa ajili ya kumuongezea.

Bosi huyo aliendelea kwa kusema: “Msimu uliopita timu zilizomtaka hazikufikia makubaliano, kwa hiyo hatukuweza kuwapa mchezaji wetu, ila sasa kama watataka kurudi tunawakaribisha.”

Kuhusu mikakati ya timu kuelekea mwisho wa msimu, Ayoub alisema: “Kwa sasa wachezaji wako mapumzikoni watarejea muda mchache kabla ya ligi kuendelea, kipindi hiki hatuna mechi yoyote ya kirafiki.”

Coastal Union inashika nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 31, imecheza mechi 28 kati ya 30, imeshinda saba, sare 10 na kupoteza 11.

Katika mechi mbili zilizobaki, Coastal inahitaji kushinda zote ili kuepuka mtegu wa kucheza mtoano kwani hivi sasa ikiteleza kidogo tu inaweza kupitwa na timu zilizopo chini yake ambazo ni Namungo yenye pointi sawa 31. Pamba Jiji (30), Tanzania Prisons (30) na Fountain Gate (29).

Wagosi hao wanamaliza msimu wakiwa nyumbani kwani mechi zilizosalia zote zitachezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga dhidi ya Fountain Gate (Juni 18) na Tabora United (Juni 22).

Rekodi zinaonyesha katika duru la kwanza, Coastal Union ilifungwa 3-2 na Fountain Gate huku ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Tabora United.