Zoran afichua ishu ya Bocco

Muktasari:
- KIKOSI cha Simba kimeondoka alfajiri ya jana kwenda Sudan kuchukua mbinu za CAF, lakini Kocha Zoran Maki amefichua siri ya kukosekana kwa nahodha wa timu hiyo, John Bocco katika mechi mbili za kwanza za Ligi Kuu Bara akisema ilitokana na kukosa utimamu wa mwili.
KIKOSI cha Simba kimeondoka alfajiri ya jana kwenda Sudan kuchukua mbinu za CAF, lakini Kocha Zoran Maki amefichua siri ya kukosekana kwa nahodha wa timu hiyo, John Bocco katika mechi mbili za kwanza za Ligi Kuu Bara akisema ilitokana na kukosa utimamu wa mwili.
Bocco hakuwepo kikosini wakati Simba ikiishindilia Geita Gold kwa mabao 3-0 kisha kuinyoosha Kagera Sugar mabao 2-0 na kuifanya timu hiyo ikae kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi sita sawa na Yanga na Singida Big Stars, lakini ikibebwa na uwiano mzuri wa mabao dhidi ya wapinzani wao.
Kocha Zoran alisema Bocco ambaye ni mchezaji wa zamani wa Azam, tayari alikuwepo katika mazoezi na ameanza kuwa fiti.
Alisema Bocco hakutumika kwenye mechi hizo mbili zilizopita ila alikuwa anafanya mazoezi pamoja na wenzake na sasa yupo fiti yupo katika orodha ya wachezaji waliokwenda Sudan alfajiri ya leo kwa ajili ya kucheza michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa.
“Bocco atacheza michezo miwili ya kimataifa kirafiki dhidi ya Asante Kotoko na Al Hilal kwa ajili ya kuongeza utimamu wake wa mwili na mara baada ya kurejea awepo katika michezo ya kimashindano,” alisema Zoran na kuongeza;
“Kabla ya kwenda Sudan Bocco alikuwa akifanya mazoezi vizuri pamoja na wachezaji wenzake waliobaki akiwa katika kiwango bora na hilo ni jambo zuri kwa timu kuwepo na mchezaji aina yake akiwa fiti,”
“Uwepo wake katika kikosi unanipa machaguo mapana ya nafasi anayocheza kwani kwa sasa watakuwepo wanne pamoja na Dejan Georgijevic, Moses Phiri ambaye anaweza kucheza nafasi nyingine na Habibu Kyombo.
“Dejan amefunga katika mchezo wa ligi uliopita hali na morali yake itakuwa juu kutamani kufanya hivyo katika michezo inayo na kwenda kucheza michezo hii ya kirafiki ataendelea kujengeka na kuzoea mazingira na timu.”
Katika hatua nyingine Zoran alisema Phiri kiasili si straika moja kwa moja ila amekuwa akitumika hapo tangu akiwa na Zambia na kwenye mechi mbili ndani ya Simba akicheza nafasi hiyo amefanya vizuri akifunga mabao mawili.
Alisema Phiri amefanya vizuri katika nafasi hiyo akionyesha kiwango bora lakini anaweza kucheza akitokea pembeni au nyuma ya mshambuliaji.
“Kyombo amekuwa akifanya vizuri katika kila mechi na naamini itakuwa hivyo katika michezo ijayo. Urejeo wa Bocco nae atatamani kufanya vizuri kama waliokuwepo katika nafasi hiyo kwa maana hiyo ubora wao utaleta ushindani na kila ambaye atapata nafasi ya kucheza atafanya vizuri,” alisema Zoran ambaye mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika atakiwasha wikiendi ya kwanza ya Septemba dhidi ya Nyanza ya Malawi.