Wachezaji wapewa masharti magumu

WAKATI baadhi ya klabu nchini zikianza mazoezi ya pamoja na kueleza namna wanavyochukua tahadhari dhidi ya corona, Chama cha Madaktari wa Michezo (TASMA) kimetoa muongozo wa mazoezi hayo na namna walivyojipanga wakati wa mechi.
Mwenyekiti wa Tasma, Dk Paul Marealle ameiambia Mwanaspoti; “Suala la kuwapima maambukizi ya corona linafanyiwa kazi na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) itaeleza Ligi itakavyoanza.”
Kuhusu tahadhari kwenye mazoezi ya pamoja ambayo baadhi ya klabu zimekwishaanza, alisema tayari wametoa muongozo kwa kuzungumza na madaktari wa klabu.
“Kupeana nafasi au kuvaa barakoa uwanjani hakuna, hivyo ni wachezaji wenyewe kuwa makini na kila mmoja kujilinda na kumlinda wenzake,” alisema Dk Marealle na kuongeza;
“Madaktari wa klabu tumekwishazungumza nao, wanajua nini cha kufanya, pia vyumba vya kubadilishia nguo uwanjani tumesisitiza lazima viwe na sanitaiza kwani kila majimaji yana matatizo yake,” alisema.
Tayari klabu baadhi ikiwamo Simba, Namungo, KMC, Polisi Tanzania na Yanga zimeanza mazoezi ya pamoja baada ya Serikali kuruhusu ziendelee na mazoezi lakini kwa tahadhari.
Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema; “Baada ya kauli za serikali, TFF hawajatoa tamko wala utaratibu wowote, hivyo tunangoja kauli yao ili tuanze mazoezi ya pamoja. “Baada ya tarehe iliyopangwa kuanza kwa michezo ndipo tutaona namna ya kuwarejesha wachezaji wetu kambini.”
Katibu wa Namungo FC, Ali Seleman alisema; “Tunachokifanya ni kuhakikisha tunachukua tahadhari zote kwa wachezaji na makocha ili kuwaweka katika mazingira salama zaidi wakati tukingoja muongozo kutoka TFF.”
Lakini Makamu Mwenyekiti wa Coastal Union, Hassan Muhsin alisema; “Hatujui chochote ndio maana tumechelewa kuwaita wachezaji kambini, hivyo Jumatatu ndio tunaanza rasmi mazoezi, tukiamini tutakuwa tumepata muongozo.”
Robert Munisi Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Polisi Tanzania ambao walianza mazoezi tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema hakuna muongozo walioupata zaidi ya kuwatumia wataalamu wao wa afya kuhakikisha wachezaji wanakuwa kwenye mazingira salama.
Lakini Mtibwa Sugar, Kocha Mkuu wake, Zubeiry Katwila alisema, bado hawajaanza kambi ila wamewataarifu wachezaji wao kabla ya Jumamosi wawe wamerejea ili kuanza kambi.
Nao mabosi AFC Arusha inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) wamesema bado hawajaingiza wachezaji kambini wakisubiri maelekezo ya TPBL juu ya tarehe hasa ya kuendelea kwa ligi, ili kuepuka gharama.
Alisema mbali na kupata tarehe pia hawajapata maelekezo yoyote kutoka Bodi ya Ligi kuhusu kujikinga na corona, licha ya kusikia wanatakiwa kuanza mazoezi tu, ila watahoji baadaye watakapoletewa barua za kuanza rasmi kwa ligi hiyo.
AFC ipo nafasi ya sita katika Kundi B ikiwa na alama 25 huku kinara wao Gwambina FC ikisaka pointi tatu watinge Ligi Kuu msimu ujao kwani ina alama 40 na kama ikifikisha 43 hazitafikiwa na timu yoyote.
Imeandikwa na Imani Makongoro, Yohana Challe, Clezencia Tryphone na Bertha Ismail