Viwango bora Serengeti Boys vyamchanganya kocha

Muktasari:
Akizungumzia kikosi chake kwa ujumla, Milambo amesema kuwa mazoezi waliyoyafanya mkoani Arusha yamewajenga wachezaji wake na wanaamini wataenda kutoa ushindani wa hali ya juu nchini Uturuki kwenye michuano ya UEFA Assist.
ARUSHA. HAZINA kubwa ya wachezaji waliojiwekea Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwenye kikosi cha Serengeti Boys imekuwa kama mtihani kwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Oscar Milambo kufanya uteuzi kuunda kikosi cha kwanza.
Timu hiyo ya Taifa kwa vijana chini ya miaka 17 'Serengeti boys' iko kambini mkoani Arusha kuakisi hali ya hewa ya baridi kama sehemu ya maandalizi yao ya kuelekea nchini Uturuki kwa mashindano maalum ya UEFA assist yanayotarajwa kufanyika hivi karibuni
Upana wa kikosi hicho chenye jumla ya wachezaji 60, imekuwa kama mtihani kwa kocha mkuu wa Serengeti boys Oscar Milambo na kusema kuwa Makali ya kila mchezaji kwa ajili ya kujitafutia nafasi ya kikosi cha kwanza ni makubwa hali inayomuweka katika wakati mgumu kupanga kikosi mapema.
"Hadi sasa bado sijapanga wachezaji wa kikosi cha kwanza wala cha pili na napata wakati mgumu wa kufanya hivyo kutokana na idadi kubwa ya wachezaji niliyonao lakini uwezo binafsi wa kila mmoja ni changamoto nyingine maana wako wanaocheza nafasi moja zaidi ya wawili au watatu na kila mmoja ana uwezo wa hali ya juu"
Amesema kuwa vijana walioko chini yake wengi wana vipaji vya kuzaliwa hivyo kuwa wabunifu wakubwa katika nafasi aliyowapanga huku mafunzo yakizidi kuwaimarisha hali ambayo inaipa asilimia kubwa Tanzania kufuzu mashindano hayo ya 'AFCON' yanayotarajiwa kufanyika hapa nchini mwezi April.
Akizungumzia kikosi chake kwa ujumla, Milambo amesema kuwa mazoezi waliyoyafanya mkoani Arusha yamewajenga wachezaji wake na wanaamini wataenda kutoa ushindani wa hali ya juu nchini Uturuki kwenye michuano ya UEFA Assist.
Milambo ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau wote wa soka kutoka Arusha kwa ushirikiano makubwa wanaouonyesha kwao tangu wameingia hadi wanatarajia kuondoka kesho kwa maandalizi ya safari yao ya kwenda Uturuki.