Ushindi atua na mikwara Jangwani

STAA aliyefungia dirisha la usajili wa Yanga, Chico Ushindi juzi usiku alitua jijini Dar es Salaam kimyakimya kisha akasafirishwa hadi Tanga na akatambulishwa kwa mashabiki kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga, huku akipiga mkwara mzito kwamba amekuja kukoleza moto Jangwani.

Winga huyo anayetumia miguu yote na anayemudu kucheza kama mshambuliaji pia ametua Jangwani kwa mkopo akitokea TP Mazembe ya DR Congo na alitambulishwa sambamba na aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba, Mbrazil Milton Nienov kabla ya mchezo wao na Coastal Union uliopigwa Mkwakwani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ushindi, aliwatumia salamu mashabiki wa Yanga akiwaambia wasiwe na wasiwasi kwani kelele za watani wao Simba wanaodai jamaa alikuwa anakaa benchi Mazembe zitakwisha kwa kazi atakayoifanya uwanjani.

Ushindi alisema, akili yake imeshajiandaa kuitumikia Yanga na kwamba anajua kila kitu anachotakiwa kukiongeza katika kikosi cha vinara hao wa Ligi Kuu Bara.

Mshambuliaji huyo anayetokea pembeni alisema amefanya mazungumzo na kocha wa Yanga, Nesreddine Nabi na amemtaka kuja kuongeza kasi ya upatikanaji wa mabao akitokea pembeni.

“Kocha (Nabi) alinipigia simu nikiwa bado Congo na akaniambia kitu gani anataka nifanye hapa Yanga nimefurahia mazungumzo yangu na kocha ,” alisema Ushindi.

“Sina wasiwasi na uwezo wangu wala hicho anachotaka nifanye jambo zuri nakuja kwenye timu yenye wachezaji wakubwa waliokomaa kiakili najua kushambulia kutoka pembeni.

“Naweza kufunga na zaidi kutengeneza nafasi wenzangu wengine wacheze wafunge tukicheza kwa ushirikiano mambo yatakuwa rahisi.”