Simba wote kambini haraka, kumkosa Kanoute

Muktasari:
- Katika mazoezi Simba itawakosa pia walioomba ruhusa za kwenda kwao ikiwemo, Sadio Kanoute ambaye bado anafuatilia suala lake la hati ya kusafiria.
WACHEZAJI wa Simba walipewa mapumziko ya siku tatu na watarejea mazoezini leo Jumatano kwa wale ambao hawapo kwenye kambi ya timu ya Taifa.
Katika mazoezi Simba itawakosa pia walioomba ruhusa za kwenda kwao ikiwemo, Sadio Kanoute ambaye bado anafuatilia suala lake la hati ya kusafiria.
Mwanaspoti linajua katika kipindi hichi ligi ikiwa imesimama Simba ilipokea mualiko kutoka kwa Al Hilal ya Sudan ambayo imeanzisha shindano la wiki moja kama maandalizi ya msimu ujao kwao pamoja na Ligi ya mabingwa Afrika lakini imeshindwa kwenda kutokana na kutokuwa na wachezaji muhimu. Katika kuhakikisha Simba inaendelea vizuri na maandalizi kwa wale wachezaji waliobaki nchini, Pape Sakho, Moses Phiri, Pater Banda, Ally Salim, Israel Mwenda, Jimsony Mwanuke na Gadiel Michael wote wataanza tizi.
Wengine John Bocco, Dejan Georgijevic, Henock Inonga, Joash Onyango, Erasto Nyoni, Victor Akpan na kuongeza wachezaji wengine kutoka timu ya vijana watacheza na mechi za kirafiki nyepesi kujiweka sawa.
Kocha wa Simba, Zoran Maki alisema; “Natamani kuona washambuliaji na wanaokutana na nafasi za kufunga wanazitumia kufunga mabao mengi na tutalifanyia kazi wakati huu wa mazoezi.”