Simba waibua mazito mkataba wa GSM na TFF

Simba waibua mazito mkataba wa GSM na TFF

Dar es Salaam. Uongozi wa Simba umepanga kugomea kuvaa jezi zenye nembo ya mdhamini mwenza wa Ligi Kuu, kampuni ya GSM kwa madai ya kutokuwepo kwa uwazi wa mkataba kati ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kampuni hiyo uliosainiwa mwezi uliopita.

 Uamuzi huo wa Simba umekuja kufuatia kile kilichotajwa na uongozi wa timu hiyo katika barua rasmi waliyoiandika kwenda kwa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) kuwa haiwezi kutekeleza sharti walilowekewa la kuvaa nembo ya kampuni ya GSM kuanzia katika mchezo dhidi ya Yanga, Jumamosi jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Katika barua hiyo iliyoelekezwa kwa mtendaji mkuu wa TPLB, Almas Kasongo, Simba wanahitaji ufafanuzi wa masuala kadhaa katika mkataba huo kabla ya kukubali agizo la bodi ya ligi kuweka nembo ya GSM kwenye jezi zao.

Miongoni mwa hoja kuu za Simba ni kuwa kitendo cha GSM kuwa mdhamini mwenza wa ligi kinatia shaka ya kutokuwepo kwa usawa kwa vile kuna mgongano wa kimaslahi baina ya kampuni hiyo na Yanga ambayo pia wanaidhamini na moja ya malengo makuu ya kampuni hiyo ni kuhakikisha klabu hiyo inatwaa ubingwa lakini pili ni usiri wa TFF katika kuzijulisha klabu juu ya hafla ya kusainiwa mkataba huo huku kundi kubwa la viongozi na maofisa wa Yanga wakihudhuria pasipo kuwepo na dhana ya usawa kwa klabu nyingine.

Mbali na hizo, Simba pia wanataka ufafanuzi wa ni kwa namna gani mkataba huo hautoziathiri klabu nyingine ukizingatia makamu mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya usajili ya Yanga, Mhandisi Hersi Said pia amekuwa akiiwakilisha GSM katika shughuli mbalimbali na amekuwa akiambatana na viongozi wa klabu hiyo jambo ambalo Simba ina wasiwasi kuwa Yanga ndio inaidhamini TPLB kwa mwavuli wa udhamini.

“Tunaamini kwamba Yanga itakuwa na faida isiyo na usawa katika TPLB nje ya uhusiano wao na GSM kama mdhamini wa kawaida tofauti na ilivyo kwa Simba na timu nyingine. Tunapenda kuikumbusha TFF na TPLB kwamba kanuni za Ligi Kuu zinazuia klabu kuwasiliana na mdhamini bila idhini ya TFF.

Katika hili, Simba na klabu nyingine hazitokuwa na uwezekano wa kuwasiliana na GSM. Hata hivyo pamoja na kikwazo hicho, Yanga inawasiliana moja kwa na mdhamini GSM. Hakuna anayejua ni kwa kiasi gani hii itaathiri usawa katika kusonga mbele kwa TPLB. Kanuni ya 16 (11.1) ya Ligi Kuu 2021 inasomeka:

“Hairuhusiwi kwa klabu/mwamuzi/mchezaji kufanya mawasiliano ya moja kwa moja na mdhamini waligi bila ruhusa ya TFF kuhusu masuala yanayohusu mkataba wa udhamini. Yeyote anayekiuka atafungiwa kipindi kati ya miezi mitatu na kumi na mbili au faini ya shilingi laki tano,” inafafanua barua hiyo ya Simba ikinukuu kanuni za ligi.

Kwa mujibu wa barua hiyo, Simba ina wasiwasi kwamba Yanga ina mwanya wa kuvunja kanuni hiyo kwa mwavuli wa udhamini binafsi wa GSM, jambo ambalo litaondoa usawa kwa klabu nyingine kinyume na dhana ya usawa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

Kitendo cha Simba kuandika barua ya kuomba ufafanuzi wa mkataba huo ni kama mwanzo wa kujivua gamba kwa klabu za soka ambazo zimekuwa na wakati mgumu kuhoji mikataba ya udhamini wa ligi ambayo TFF imekuwa ikiingia na kampuni na taasisi mbalimbali.

Licha ya TPLB kuwa chombo ambacho kinasimamia maslahi ya klabu, hali imekuwa tofauti kwani TFF ndio imekuwa ikisaini makubaliano ya mikataba ya udhamini wa ligi huku klabu za soka zikiwa hazishirikishwi katika majadiliano lakini hata kufahamu vipengele vya mikataba hiyo.

Hata hivyo, mara baada ya kusainiwa mkataba huo mwezi uliopita, TFF ilitoa onyo kwa wadau wa soka na klabu kutoa ufafanuzi juu ya mkataba huo.

“Tunapenda kusisitiza kuwa mkataba huo wa miaka miwili ni kati ya TFF na GSM Group. Hivyo hakuna klabu wala mtu anayeweza kutolea ufafanuzi mkataba huo zaidi ya pande husika.

“TFF haitosita kuchukua hatua dhidi ya klabu ambazo zinajaribu kutolea ufafanuzi au kuelezea mkataba huo wakati wahusika ni TFF na GSM Group,” ilifafanua taarifa ya TFF.

Katibu wa KMC FC, Walter Harisson alisema wamepokea barua kutoka Bodi ya ya udhamini wa GSM na wanapitia vifungu vilivyomo ndani ya mkataba huo kisha watazungumza.

Naye Mwenyekiti wa Biashara United, Seleman Matasso alisema wao wanachotaka ni pesa mengine kuhusu mkataba huo hayawahusu.