Simba, Chama moto umewaka

Picha ikiwaonyesha viongozi wa Simba wakiwa pamoja na wazazi wa mchezaji, Clatous Chama raia wa Zambia.
WAKATI kukiwa na taarifa tofauti juu ya kurejea wa kiungo wa zamani wa Simba, Clatous Chama raia wa Zambia, uongozi wa klabu hiyo ukiongozwa na Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez wamefanya kikao na wazazi wa mchezaji huyo baada ya mchezo wao wa marudiano na Red Arrows uliofanyika jijini Lusaka, juzi.
Barbara alisisitiza jana kwamba; “Dirisha dogo linakwenda kufunguliwa tunasubiri ripoti ya Kocha. Lakini kwa aina ya mchezo tuliouona na malengo yetu lazima tufanye maamuzi magumu sasa kwa kusajili wachezaji wazuri zaidi, ili tupate mafanikio tunayoyataka kwenye michuano hii ya Afrika.”
Simba ilimuuza Chama katika timu Berkane RBS ya Morocco lakini imeonyesha kuwa hana wakati mzuri kwenye kikosi hicho hivyo ameonyesha nia ya kutaka kuachana nao lakini klabu hizo kongwe hapa nchini Simba na Yanga kila moja imekuwa ikitajwa kutaka kumnasa nyota huyo.
Hata hivyo, upepo ni mzuri kwa Simba ambao walimuuza nyota huyo huku ikidaiwa kuwa katika makubaliano yao ya mkataba na Berkane walikubaliana kwamba endapo mchezaji huyo watataka kumuuza ama kumtoa kwa mkopo basi kipaumbele iwe timu yake hiyo ya zamani.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba,Mulamu Ng’hambi aliliambia Mwanaspoti jana akiwa Zambia kuwa, ujio wa wazazi wa Chama, baba na mama yake ni kuwasalimia wachezaji na viongozi ambao walikuwa wakiishi na mtoto wao vizuri.
Licha ya kugoma kufafanua kama wameshaanza mazungumzo siriazi ya kumrejesha mchezaji huyo kundini lakini alisisitiza kwamba; “Kama Chama atarudi Tanzania atakuja kucheza Simba, hawezi kwenda Yanga wala klabu nyingine nisikilize mimi.” Pamoja na kauli hiyo, lakini Mwanaspoti linajua kwamba Yanga nao wako kwenye mazungumzo na vigogo wa Berkane na wakala wa Chama kuhakikisha wanamnasa mchezaji huyo. Chama kwenye mahojiano yake maalum na Mwanaspoti wiki iliyopita alisisitiza kwamba; “Nimesikia mambo mengi kwenye mitandao lakini muda utaongea. Nikisema nizungumze kiundani zaidi yanaweza kutafsiriwa tofauti.”
Kuhusu ziara hiyo ya wazazi, Mulamu alisema kuwa baada kujua Simba wanaenda Zambia walipofika walipata ugeni huo na waliwapokea wenyeji wao nchini humo na kupata nafasi ya kubadilishana mawazo ikiwemo kwenda nao uwanjani kushuhudia mchezo huo licha ya ndugu zao Red Arrows kuondolewa kwenye mashindano.
“Tulikaa nao hotelini, wao walikuja kutusalimia kama familia iliyoishi na mtoto wao Tanzania, tulifurahi sana, maana walizungumza nasi pamoja na wachezaji pia,”alisema.
Alisema mara baada ya kutoka uwanjani walirejea tena hotelini na kupata chakula cha usiku pamoja na baadae kurejea nyumbani.
Wazazi wa Chama mbali na namna ambavyo Simba waliishi na mtoto wao pia waliwashukuru viongozi kwa namna ambavyo walikuwa karibu na mtoto wao wakati wa msiba wa mke wake hadi kutuma mwakilishi kutoka Tanzania. Wakati huo huo, timu hiyo inatarajia kurejea nchini leo jioni ambapo itapokelewa na wanachama na mashabiki wao.
“Kesho jioni tunarejea na kuendelea na majukumu mengine, tunamshukuru Mungu kuingia hatua ya makundi ndiyo yalikuwa malengo yetu,”alisema.
“Hatukupata tatizo lolote hata pale uwanjani wakati wa mazoezi siku moja kabla ya mchezo ilikuwa ni mambo ya taarifa tu, mlinzi aliambiwa asiingie mtu uwanjani na hata sisi tulipofika hakujua kama ni wageni lakini baadae tuliingia na kuendelea na majukumu yetu kama kawaida,” alisema.
KUHUSU YANGA
“Hili gari limeshawaka sisi hatuzuwiliki tena, sasa tunataka ubingwa wa Afrika. Mechi ya Yanga tunakwenda kucheza kama mechi zingine,”alisema Salim Try Again Mwenyekiti wa Bodi ya Simba.
PABLO AFUNGUKA
Kocha wa Simba, Pablo Franco alisema; “ Dhidi ya Yanga malengo ni kupata ushindi kama hizo nyingine.
“Mechi ya Dabi katika nchi yoyote ile huwa ni kubwa na ushindani wa kutosha kwahiyo hata hiyo itakuwa hivyo hivyo kulingana na wachezaji wangu walivyo naimani tunakwenda kufanya vizuri kwa kuondoka na ushindi,”
“Kufanya vizuri mechi tatu chini yangu inaongeza hali na morali ya wachezaji kwenye kushindana katika mechi hiyo,”aliongeza Kocha huyo.