Sababu Bocco, Mauya kuachwa Taifa Stars

Sababu Bocco, Mauya kuachwa Taifa Stars

Dar es Salaam. Wakati viungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Himid Mao wakirudishwa katika kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’, benchi la ufundi la timu hiyo limedai sababu ya baadhi ya wachezaji kutojumuishwa ni kutokana na kushindwa kufikia mahitaji ya kiufundi.

Licha ya kufanya vizuri katika siku za hivi karibuni, kiungo Zawadi Mauya wa Yanga; mwenzake wa Simba, Mzamiru Yassin na mshambuliaji John Bocco hawajaitwa katika kikosi cha Stars kilichotangazwa jana kwa ajili ya michezo miwili ya kuwania kufuzu Fainali za Matifa ya Afrika (Afcon) mwakani dhidi ya Algeria na Niger.

Kwa mfano Bocco ambaye kwa muda mrefu msimu huu alikuwa na ukame wa mabao amefunga mabao matatu katika mechi tatu mfululizo zilizopita za Ligi Kuu dhidi ya Azam, Kagera Sugar na Ruvu Shooting.

Mbali na watatu hao, wengine ambao hawajaitwa ni Israel Patrick na Jonas Mkude (Simba), Lusajo Mwaikenda na Tepsi Evance (Azam) pamoja na Abdulrazack Hamza (Namungo FC).

Kocha msaidizi wa Stars, Shadrack Nsajigwa alisema kuwa sababu kubwa iliyofanya kuwaacha baadhi ya nyota ni za kiufundi ingawa bado wana nafasi kikosini siku za usoni.

“Wachezaji ambao hatujawaita safari hii kuna sababu mbalimbali na wengine ni baada ya benchi la ufundi kutoridhika na kile walichokionyesha kwenye mechi za awali, lakini wakifanya vizuri watarudi,” alisema Nsajigwa.

Wakati nyota hao wakifungiwa milango walau kwa muda katika kikosi cha Stars, kiungo wa Yanga, Salum Abubakar, nyota wa Ghazl El Mehalla, Himid Mao na beki wa kati wa Azam FC, Abdallah Kheri wamerudishwa kundini.

Nsajigwa alisema kuitwa kwa wachezaji hao kumetokana na viwango ambavyo wamevionyesha kwenye klabu zao.

“Mao awali hakuwa kwenye kikosi kwa sababu eneo lake kulikuwa na wachezaji wengine. Yeye ameingia baada ya kumfuatilia na kuridhika na uwezo wake. Hatujamuita kisa watu walikuwa wanaongea bali ni uwezo wake,”alisema Nsajigwa.

Nyota wa zamani wa Simba na Yanga, Zamoyoni Mogela alisema ingizo la Sure Boy na Mao kikosini ni zuri na hajashangazwa kuachwa kwa Bocco.

“Bocco alikuwa na panda shuka hapa katikati mpaka mashabiki wa timu yake walikuwa wanasema, kwa sasa kweli anafanya vizuri lakini kuna utimamu wa mwili pia nao unachangia,” alisema.

Wachezaji walioitwa ni Aishi Manula, Metacha Mnata, Abuutwalib Mshery, Shomari Kapombe, Kibwana Shomari, Mohamed Hussein na Haji Mnoga.

Nickson Kibabage, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Abdallah Kheri, Kennedy Juma, Novatus Dismas, Mzamiru Yassin na Aziz Andambwile.Himid Mao, Sure Boy na Simon Msuva.

Wengine ni Kelvin John, Mbwana Samatta, Farid Mussa, Abdul Suleiman na Feisal Salum, Ben Starkie, Lusajo Mwaikenda, Kibu Denis, George Mpole na Ibrahim Joshua.