Prime
Waarabu watia mkono Yanga

Muktasari:
- Nyota huyo anayemaliza mkataba na TP Mazembe Juni 30, 2025, inaelezwa hivi karibuni atatua hapa nchini kwa ajili ya mazungumzo na Yanga kuhusu maslahi binafsi, japo kitendo cha Esperance kujitokeza kumhitaji huenda kikatibua dili hilo.
WAKATI Yanga ikijiandaa kumleta nchini beki wa kulia wa TP Mazembe na timu ya taifa ya Mauritanian, Ibrahima Keita, dili hilo limeanza kuingia gundu baada ya matajiri wa Tunisia kuingilia kati.
Nyota huyo anayemaliza mkataba na TP Mazembe Juni 30, 2025, inaelezwa hivi karibuni atatua hapa nchini kwa ajili ya mazungumzo na Yanga kuhusu maslahi binafsi, japo kitendo cha Esperance kujitokeza kumhitaji huenda kikatibua dili hilo.
Kwa mujibu wa Gazeti la Tunisia, La Presse, mabingwa wa Ligi Kuu ya Tunisia, Esperance wapo tayari kumsajili beki huyo kwa kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya msimu ujao wa michuano ya Ligi Kuu ya Tunisia ‘Ligue Professionnelle 1’ na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mbali na Keita anayewindwa na kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao, mastaa wengine ni mshambuliaji raia wa Algeria, Baghdad Bounedjah kutokea Al-Shamal ya Qatar na beki wa kati, Dylan Bronn anayeichezea US Salernitana 1919 ya Italia.
Keita ni miongoni mwa mabeki wanaowindwa sana na Yanga baada ya beki wa kulia wa kikosi hicho, Yao Kouassi kutokuwa fiti kwa kipindi hiki, kutokana na kufanyiwa upasuaji wa goti la kushoto, ikiwa ni baada ya kupona jeraha la kifundo cha mguu.
Yao aliyejiunga na Yanga msimu wa 2023-24, akitokea ASEC ya Ivory Coast, ameonyesha kiwango bora hadi sasa na kikosi hicho, japo majeraha ya mara kwa mara yakiwamo ya nyama za paja yanawafanya mabosi kuangalia tena mbadala wake.
Tangu alipoumia, beki tegemeo wa kulia ni Israel Mwenda aliyejiunga dirisha dogo la Januari 2025, akitokea Singida Black Stars, viongozi wanahitaji kumpata Ibrahima anayepatikana bure mwishoni wa msimu huu ili kuongeza ushindani.
Hata hivyo, gazeti la Mwanaspoti linatambua Yao mkataba na Yanga unaisha mwisho wa msimu huu, ingawa viongozi wa timu hiyo wapo tayari kumuongezea mmoja zaidi, japo watamtoa katika mfumo wa usajili ili kutoa nafasi kwa nyota wengine waliopo fiti.