Prime
Hatuchezi yachukua sura mpya

Muktasari:
- Bodi ya Ligi iliahirisha mechi mechi awali muda mfupi baada ya Simba kutishia kuichezea kwa madai ya kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho Kwa Mkapa na wanaodaiwa makomandoo wa Yanga, huku ikielezwa kulikuwa na vitu vilivyoashiria hali ya usalama iliyokuwa ikichunguzwa.
MSISITIZO wa Yanga wa kutocheza Dabi ya Kariakoo bado upo palepale. Inaelezwa kuwa Yanga, haitacheza Dabi ya Kariakoo Juni 15 mwaka huu dhidi ya Simba hadi haki yao ipatikane baada ya mechi hiyo kuahirishwa awali Machi 8.
Bodi ya Ligi iliahirisha mechi mechi awali muda mfupi baada ya Simba kutishia kuichezea kwa madai ya kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho Kwa Mkapa na wanaodaiwa makomandoo wa Yanga, huku ikielezwa kulikuwa na vitu vilivyoashiria hali ya usalama iliyokuwa ikichunguzwa.
Hata hivyo, kabla ya kutolewa majibu ya yaliyosababisha dabi hiyo kuahirishwa, Bodi ilitangaza tena kwamba mechi hiyo itapigwa Juni 15 na Yanga kusisitiza haitakuwa tayari kucheza hadi malalamiko yao ya kuahirishwa kienyeji kwa mechi ya Machi 8 wapatiwe majibu.
Taarifa mpya zilizoibuka mara baada ya Bodi kutangaza tarehe hiyo mpya ni kwamba siku hiyo ya Juni 15, Yanga itakuwa Kigali kuvaana na Rayon Sports kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa.
Rais wa Rayon Sports, Thadée Twagirayezu amezungumza na Mwanaspoti moja kwa moja kutoka Rwanda na kufichua jambo hilo.
Katika mahojiano hayo maalum, Rais huyo aliyeingia madarakani Novemba 2024 baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo, alisema ni kweli wapo katika mazungumzo na uongozi wa Yanga kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki kutokana na ushirikiano walionao.
Rais huyo alibainisha kuwa, mazungumzo hayo kama yataenda vizuri, basi watacheza dhidi ya Yanga Julai mwaka huu katika Tamasha la Rayon Sports Day, lakini sio Juni 15 kama inavyoelezwa.
“Kwa sasa tumemaliza msimu na wachezaji wameenda kwao baada ya kuvunja kambi,” alisema Twagirayezu na kuongeza;
“Tunatarajia kuanza maandalizi ya msimu ujao mapema, hivyo Juni 15 watu waanze kurudi kambini kisha ndio tuanze maandalizi. Unajua sisi ni timu ya Wananchi, tumekuwa na uhusiano mzuri na Yanga ambao pia ni Wananchi, hivyo tungependa tucheze nao katika Rayon Sports Day hiyo Julai.”
Ikumbukwe kuwa, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imepanga Juni 15 mwaka huu ichezwe mechi ya kiporo Yanga dhidi ya Simba baada ya kuahirishwa Machi 8.
Yanga imeonekana kutokubaliana na ratiba hiyo mpya huku ikitaka maelezo ya kina sababu za kuahirishwa awali licha ya kwamba TPLB ilizitaja ikiwamo madai ya Simba kuzuiwa kufanya mazoezi uwanja wa mechi siku moja kabla.
Madai ya Yanga juu ya kusaka haki yao hayakuishia mamlaka za soka za ndani pekee, bali yalifika hadi Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) nchini Uswisi, lakini shauri lao liliondolewa na kutakiwa kurudi katika mamlaka za ndani, ambapo haikukubaliana na hilo ikaamua kutocheza.
Wakati Yanga ikiendelea na msimamo huo, TPLB imeendelea kusisitiza mechi ipo kama ilivyopangwa na Simba inaendelea na maandalizi ya mchezo huo ikiwa ni timu ngeni baada ya ile ya duru la kwanza katika Ligi Kuu Bara kufungwa 1-0.
“Ratiba tumeshapanga, tusubiri siku ifike,” amesema kwa ufupi Mwenyekiti wa TPLB, Steven Mguto alipoulizwa kuhusu uwepo wa mchezo huo.
Mchezo huo kwa kiasi kikubwa umeshikilia ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kufuatia hivi sasa Yanga kuwa kileleni na pointi 73, ikkfuatiwa na Simba yenye 72, huku kila upande ukicheza mechi 27 na kubaki tatu.
Yanga katika mechi tatu zilizobaki ni dhidi ya Simba (Juni 15 nyumbani), Tanzania Prisons (Juni 18 ugenini) na Dodoma Jiji (Juni 22 nyumbani).
Simba mechi tatu ni dhidi ya Yanga (Juni 15 ugenini), KenGold (Juni 18 ugenini) na Kagera Sugar (Juni 22 nyumbani).
Endapo Yanga itaendelea kushikilia msimamo wa kutocheza huku ratiba ikaendelea kama kawaida, maana yake itakabiliwa na adhabu ya kukatwa pointi 15 na faini na kuiachia Simba ubingwa ikiubeba kwa mara ya kwanza baada ya kuukosa misimu mitatu mfululizo. Pia itakuwa mara ya 23 katika historia ya klabu hiyo wakti Yanga inaongoza kwa kubeba mara 30.
Kwa kukatwa pointi 15, Yanga itakuwa nazo 58 huku ikilazimika kushinda mechi mbili za mwisho ili kufikisha 64 zitakazoifanya kumaliza nafasi ya pili.
Lakini kama mchezo ukafanyika kama ulivyopangwa, basi matokeo ya ushindi upande wowote yatatoa picha ya nani anaukaribia ubingwa.