Nabi: Nataka muwapige nyingi

PAMOJA na Yanga kuanza kwa ushindi wa mabao 2-1 msimu huu na kuendeleza rekodi ya kutofungwa kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi amesema anahitaji mabao mengi zaidi hivyo anamechi tatu ambazo ni sawa na dakika 270 kuhakikisha safu ya kiungo inakuwa na uelewano mzuri na washambuliaji.
Yanga ilicheza mchezo wa ngao ya jamii na watani zao Simba ikishinda mabao 2-1 huku ikiendelea ya rekodi ya kutofungwa kwenye mechi za ligi kwa kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania ugenini.
Nabi amesema anakikosi kizuri lakini eneo la ushambuliaji na viungo wanaotoa asisti akimlenga zaidi Stephen Aziz KI bado hawana maelewano mazuri hivyo wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi lakini wanashindwa kuzitumia.
“Kwenye michezo yote miwili Ngao na ligi nafasi nyingi zimetengenezwa lakini tumepata mabao mawili tu nimebaini kuwa sababu kubwa ni kukosa muunganiko na maelewano mazuri kwa washambuliaji na viungo,” alisema na kuongeza;
“Aziz KI ni mchezaji mzuri kwenye kutengeneza nafasi pamoja na kufunga akitengeneza pacha nzuri na washambuliaji hasa Fiston Mayele na Heritier Makambo watafunga sana ukirudia mechi mbili tulizocheza utaona ni pasi ngapi za mwisho ametoa na ngapi zimetumika.”
Nabi alisema kwenye uwanja wa mazoezi tayari ameshaanza kulifanyia kazi hilo ili kuhakikisha wanakuwa na idadi kubwa ya mabao msimu huu kutokana na aina ya wachezaji walioongezwa kikosini pamoja na washambuliaji alionao na anatarajia mabadiliko dhidi ya Coastal Union leo jioni jijini Arusha.
“Kuna kila sababu ya kutumia kila nafasi inayotengenezwa hii ni kutokana na aina ya wachezaji nilionao nitahakikisha safu yangu ya ushambuliaji inakuwa bora zaidi msimu huu nina wachezaji wazuri wanaoweza kupiga pasi za mwisho ukiangalia safu yangu ya kiungo inatengenezwa na wachezaji wazoefu wengi,” alisema.
Yanga imepania pia kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa msimu huu ikipangwa kuanzia Sudan Kusini.