Nabi ataja siku ya ubingwa

Friday May 20 2022
Nabi PIC
By Thobias Sebastian

YANGA ina dakika 270 tu za uwanjani za kupeleka Jangwani taji lake la 28 la Ligi Kuu Bara na kocha wa vinara hao, Nasreddine Nabi ameitaja Juni 22 kuwa ndio siku ya kukamilisha furaha ya Wananchi.

Vigogo hao ambao wameongoza ligi kwa takribani msimu huu wote kufikia sasa wakiwa na pointi 60, wamebakiza mechi sita kumaliza msimu, lakini wanahitaji pointi 9, ili kufikisha pointi 69 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote ikiwamo Simba ambayo jana ilitoka sare ya 1-1 na Azam FC.

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, ambaye alikuwapo uwanjani Azam Complex jana kuwasoma Simba kwa mechi yao ya nusu fainali ya Kombe la ASFC, alisema anataka kuona timu yake inatwaa ubingwa haraka iwezekanavyo na jambo hilo linaweza kufanikiwa Juni 15 katika mechi yao ya tatu kuanzia sasa dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Nabi alisema halitakuwa jambo la kawaida kwao kuanza msimu wakiwa wanafanya vizuri na washindwe kumaliza kwenye ubora huo na bahati nzuri wachezaji wake wote wamemuhakikishia hilo.

Alisema kuanzia kwenye uwanja wa mazoezi na maisha yao ya kambini kila mchezaji amemueleza wanakwenda kupambana na kuhakikisha wanafanya vizuri kwa kushinda mechi hizo nne kabla ya kucheza mechi zao tatu za mwisho dhidi ya Polisi Tanzania Dar es Salaam, Mbeya City ugenini Sokoine, Mbeya na dhidi ya Mtibwa Sugar Kwa Mkapa.

“Jambo la faraja kwangu kuona napata nguvu ya kutosha kutoka kwa viongozi, wachezaji ambao wameonyesha kuwa na njaa ya mafanikio inakuwa rahisi kwangu kuwaelekeza yale ya kufanya katika mazoezi na mechi ili mwisho wa siku tufikie malengo ya kupata ushindi,” alisema Nabi na kuongeza;

Advertisement

“Ambacho tunafanya wakati huu kwenye uwanja wa mazoezi ni kufanya mazoezi mengi ya mbinu, kupunguza makosa yetu kwa kuangalia mechi iliyopita pamoja na kuimarisha ubora tulionao ili kushinda na kucheza mpira wa kuvutia.

“Mara nyingi mazoezi ya mbinu ambayo tunafanya yanalingana na wapinzani tunaoenda kukutana nao, bahati nzuri timu sita tulizobaki kucheza nazo, kwenye mzunguko wa kwanza nyingi tulipata matokeo mazuri dhidi yao kwahiyo tunawafahamu.”

Katika hatua nyingine Nabi alisema kikosi cha Yanga msimu ujao kitakuwa na makali zaidi kwani kuna mambo ya msingi kiufundi msimu huu hayakwenda vizuri kulingana na sababu za nje ya uwezo wake.

“Yanga hii ya sasa mbali ya kuonekana kuwa kali, bado haijafikia pale nilipokuwa nahitaji kuona inakuwa tishio ndani na nje ya nchi,” alisema Nabi na kuongeza;

“Kati ya sababu ni kwamba timu ilikuwa na wachezaji wapya wengi na hatakuwa na muda wa kutosha wa maandalizi (pre season), sababu tulianza moja kwa moja kucheza mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika. Lakini mara hii tutaingia sokoni mapema kutafuta wachezaji wengine imara na wenye uwezo ili wakikutana na waliopo sasa waongeze ubora wa timu.”

Yanga wamebakiwa na mechi sita dhidi ya Mbeya Kwanza (H), Biashara, Coastal Union (H), Polisi Tanzania (H), Mbeya City (A) na Mtibwa Sugar (H).

Kwenye mzunguko wa kwanza dhidi ya timu hizo sita, Yanga ilishinda mechi tano na kutoka suluhu moja tu na Mbeya City.

Advertisement