Nabi apindua meza kibabe, Amuachia msala Pablo

KOCHA wa Yanga, Nesreddine Nabi ametegua mitego, iliyoikwamisha timu hiyo kulikosa taji la Ligi Kuu Bara msimu uliyopita na kumuachia msala kocha wa Simba, Pablo Franco.
Yanga ilianza kuondoka kwenye ramani ya ubingwa, baada ya kuchapwa na Coastal Union ya Tanga, mabao 2-1, huku winga wao Tuisila Kisinda akikosa penalti iliyookolewa na kipa Abubakar Ibrahim dakika ya 9. Mabao ya Coastal Union yalifungwa na Erick Msagati dakika 10,Mudathir Abdallah dakika ya 83, upande wa Yanga alikuwa Kisinda, wakati huo timu ilikuwa chini ya Cedrick Kaze.
Mchezo wa pili Yanga, ilitoka sare ya bao 1-1 na Polisi Tanzania,wafungaji ni Fiston Abdul Razak dakika ya 41 na Pius Buswita dakika ya 90, matokeo yaliyomfanya Kaze kufutwa kazi na waajiri wake.
Msimu huu Nabi, ameviondoa vikwazo vya msimu ulioisha kwa kushinda mechi hizo, akikiongoza kikosi chake kikiichapa Coastal Union mabao 2-0 (Mayele dk 40, Saido dk 89) na kuifunga Polisi Tanzania bao 1-0 (Ambundo dk 64).
Wakati Nabi anategua mitego ya kukwamisha ubingwa, imekuwa tofauti kwa Pablo wa Simba ambaye amejiweka kitanzi kupoteza mechi zilizowasaidia msimu ulioisha kunyakua taji.
Coastal Union iliyochangia Yanga kuondoka kwenye ramani ya ubingwa, Simba iliifunga mabao 7-0 msimu ulioisha, huku John Bocco akifunga hat-trick dakika ya 22, 28 na 37.
Mastaa wengine walifunga mabao manne kati ya saba ni Benard Morrison dakika 46 na Clatous Chama dakika ya 59 na 85, ambapo msimu huu wamekubari kudondosha pointi mbili, wakitoka suluhu Uwanja wa Benjamin Mkapa. Ukiondoa mchezo huo, Mbeya City walioichapa mabao 4-1 msimu uliopita mabao yakifungwa na Larry Bwalya dakika 30, Luis Miquissone dakika 34, Bocco dakika 46, Chama dakika 85, huku la kufutia machozi la wenyeji wao likifungwa na Pastory Athanas dakika 50, tayari imewachapa bao 1-0.
Simba msimu ulioisha iliichapa Mtibwa Sugar, Uwanja wa Mkapa mabao 5-0 mabao yakifungwa na Chama dakika 9,Bwalya dakika 19 na Meddie Kagere dakika 44 na 51, lakini katika ligi inayoendelea wameanza kwa kudondosha pointi tatu kwa kufungwa 1-0 na Mbeya City, kisha kusuluhu na Mtibwa Sugar kabla ya juzi kulala tena 1-0 kwa Kagera Sugar. Kutokana na mwenendo wa klabu hizo,staa wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel alisema ni wakati wa Wanamsimbazi kukaza buti katika mechi zilizosalia.
“Huu ni mpira, hakimu ni dakika 90, Simba isife moyo, wapambane kushinda mechi zilizopo mbele yao,kwani lolote linaweza likatokea,”alisema.
Hoja yake iliungwa mkono na beki wa zamani wa Yanga, Samson Mwamanda aliyesema ni kweli timu yake inaongoza ligi, lakini alishauri wachezaji wasibweteke wakijua Simba ni ileile.