Mukoko aigomea Yanga, GSM aingilia kati

Monday January 17 2022
Mukoko PI
By Mwandishi Wetu

DILI la kiungo na nahodha msaidizi wa Yanga, Mukoko Tonombe kwenda TP Mazembe ya DR Congo, limekufa baada ya nyota huyo kugoma kutolewa kwa mkopo katika klabu hiyo, huku bilionea wa klabu hiyo Ghalib Mohamed ‘GSM’ akiingilia kati.

Mabosi wa Yanga walishakubaliana na mchezaji huyo kwenda Mazembe baada ya kuona hapati nafasi katika kikosi cha kwanza cha Nasreddine Nabi, pia ili kupishana na Chico Ushindi ambaye jana alitambulishwa Tanga akitokea Mazembe.

Katika dili la Yanga kumtaka Ushindi walitaka kumpeleka Mukoko na makubaliano mengine ili kumpata winga huyo mwenye spidi na uwezo wa kuitumikia vizuri nafasi hiyo na tayari Mukoko alifanyiwa taratibu zote za kusafiri kwenda DR Congo pamoja na mambo mengine ya msingi ikiwemo kutumiwa tiketi ya ndege saa 9:00 alfajiri ya Jumamosi kwenda Lubumbashi kujiunga na kikosi hicho.

Hata hivyo, Mukoko aligomea safari hiyo na kwenda kuzungumza na mdhamini wa klabu ya Yanga, bilionea Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ juu ya yote anayopitia.

Inaelezwa hatma ya katika kikao hicho kizito kati ya Mukoko na GSM, ilikuwa ni mchezaji huyo kutokwenda tena DR Congo kujiunga na Mazembe na badala yake kukatiwa tiketi ya kwenda Arusha kuisubiri Yanga iliyokuwa Tanga ikicheza na Coastal Union katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu jana Uwanja wa Mkwakwani.

Mukoko alisema mbali ya kufanya taratibu zote alishindwa kusafiri kutokana na kushindwa kufahamu hatma yake kwamba anaenda TP Mazembe kama mchezaji wa mkopo au anauzwa moja kwa moja na kumfanya amuone GSM.

Advertisement

“Bosi ameniambia nisiende kokote nitabaki hapa Yanga mpaka mwisho wa msimu utakapomalizika na baada ya hapo ndio kutakuwa na mazungumzo mengine kati yetu,” alisema Mukoko na kuongeza;

“Nimeambiwa keshokutwa nitapewa tiketi ya ndege kwenda kujiunga na timu kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania.”

Advertisement