Mrwanda: Serengeti Boys mna deni kubwa

Muktasari:
Serengeti Boys inayonolewa na Kocha Oscar Mirambo inaendelea na maandalizi yao wakitumia Uwanja wa JK Park kwa ajili ya mazoezi.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Taifa Stars pamoja na klabu za Simba na Yanga, Danny Mrwanda amewaambia madogo wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ watambue wana deni kwa Watanzania kwenye mashindano ya AFCON na wamsikilize sana mwalimu wao.
Serengeti Boys inayonolewa na Kocha Oscar Mirambo inaendelea na maandalizi yao wakitumia Uwanja wa JK Park kwa ajili ya mazoezi.
Mrwanda alisema uwakilishi wa Serengeti Boys katika mashindano hayo umekuwa deni kutokana na mambo mengi.
“Kwanza watambue Watanzania wana matumaini makubwa na wao, hivyo wanatakiwa kutowaangusha sasa hilo ni deni. Lakini, wanacheza katika ardhi ya nyumbani kwa namna yoyote wanatakiwa kuitumia nafasi hiyo kwa faida na kupata matokeo mazuri,” alisema Mrwanda.
Alisema, ili kufanikiwa hilo, vijana wa Serengeti Boys wanapaswa kumsikiliza kwa umakini mkubwa mwalimu wao na kufuata maelekezo wanayopewa.
“Unapofanyia kazi majukumu ambayo mwalimu anakupa kwa namna yoyote upo uwezekano wa kufanikiwa,” alisema Mrwanda ambaye pia alicheza soka la kulipwa nchini Malasia na Vietnam.