Mourinho awabwatukia mashabiki wa Chelsea

kocha wa Chelsea, Jose Mourinho akisaini vitabu mbalimbali vya mashabiki wake alipoanza kuifundisha timu hiyo. Picha na Maktaba
Muktasari:
Juzi Chelsea ilinusurika kutoka sare na QPR katika pambano lililopigwa uwanja wao wa nyumbani Stamford Bridge jijini London baada ya Charlie Austin kusawazisha bao la Oscar, kabla ya bao la Penalti la Eden Hazard kuipa ushindi Chelsea.
HAMFAI hata kidogo. Hamtusaidii. Ndivyo anavyolalamika kocha wa Chelsea, Jose Mourinho dhidi ya mashabiki wake wa Chelsea. Anaona wako kimya uwanjani na wanaisaidia timu pinzani.
Juzi Chelsea ilinusurika kutoka sare na QPR katika pambano lililopigwa uwanja wao wa nyumbani Stamford Bridge jijini London baada ya Charlie Austin kusawazisha bao la Oscar, kabla ya bao la Penalti la Eden Hazard kuipa ushindi Chelsea.
Lakini bila ya kujadili sana mechi, Mourinho amekerwa na tabia ya mashabiki wa timu yake kukaa kimya muda mwingi bila ya kupiga kelele za kuwasapoti wachezaji ndani ya uwanja.
“Kila mtu anajua jinsi nilivyo karibu na mashabiki wa klabu hii. Lakini kwa sasa ni vigumu kucheza mechi za nyumbani kwa sababu inakuwa kama vile mnacheza uwanja mtupu,” alisema Mourinho.
“Inapokuwa hivyo timu inaanza kucheza taratibu na soka laini nyumbani. Ni vigumu kwa timu pinzani kucheza vizuri kama wachezaji na mashabiki Stamford Bridge wote wako pamoja. Leo nilikuwa nauangalia uwanja, ilikuwa kama vile uko mtupu, sio kwa suala la idadi ya watu, hapana, ulikua umejaa ila ulikuwa kimya, hicho ndicho kinachoudhi,” alisema Mourinho.
Kocha huyo Mreno mwenye maneno mengi pia alipigia kijembe kitendo cha taa za usiku kuchelewa kuwashwa uwanjani hapo licha ya kwamba mechi hiyo ilichezwa katika mida ya jioni.
“Nadhani mtu ambaye alikuwa anahusika na masuala ya taa alikuwa katika hali kama ya mashabiki, kwa sababu kila mtu alikuwa amelala. Ilichukua dakika 20 kuelewa kuwa giza lilikuwa limeingia, lakini ilichukua dakika 30 kuelewa kuwa uwanja haukuwa mtupu.”
Chelsea inashika nafasi ya saba kwa wastani wa mashabiki katika Ligi Kuu ya England ikiwa ina wastani wa mashabiki 41,556, lakini ina mpango wa kuongeza ukubwa wa uwanja huo ili kufikia mashabiki 50,000 miaka michache ijayo.
Watarudi tena katika ligi kwenye uwanja huo mwishoni mwa mwezi huu wakati watakapoikaribisha West Brom, lakini kwa sasa wanatazamiwa kukipiga katika pambano la Ligi ya Mabingwa dhidi ya Maribor ugenini na kisha dhidi ya Liverpool katika Uwanja wa Anfield.