Mbeya Kwanza yatoa gundu Sokoine ikiilaza Mwadui

Mbeya. Kwa mara ya kwanza Mbeya Kwanza imepata ushindi katika uwanja wa Sokoine Mbeya baada ya kuichakaza Mwadui mabao 2-1 katika mchezo wa kombe la shirikisho (ASFC).
Kabla ya ushindi huo, timu hiyo ilikuwa imecheza michezo mitano katika uwanja huo bila kupata ushindi ikiwa ni sare nne na kupoteza moja ambazo ni dhidi ya Mbeya City 2-2, Dodoma Jiji suluhu, Polisi Tanzania 2-2, Biashara United 1-1 na kupoteza kwa Yanga mabao 2-0.
Leo ikitumia vyema dakika 45 za kwanza waliweza kuwachachafya wapinzani hao wanaoshiriki Championship kwa kupata mabao hayo kupitia kwa Oscar Mwajanga aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Mohamed Kapeta na kabla ya mapumziko Chrispin Ngushi akaipatia bao la pili kwa shuti kali nje ya 18.
Kipindi cha pili wenyeji walionekana kuridhika na kucheza chini ya kiwango, huku Mwadui wakionekana kubadilika na kufanya mashambulizi ya kushtukiza yaliyowasaidia kupata bao la kujifutia jasho lililofungwa na Washa Machungwa dakika ya 85.
Kwa matokeo hayo Mbeya Kwanza inafuzu hatua ya 34, huku Mwadui wakitolewa na sasa akili na nguvu kuelekezwa kwenye Ligi ya Championship kusaka kubaki au kupanda Ligi Kuu msimu ujao.
Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza, Hererimana Haruna amesema licha ya matokeo hayo, lakini vijana wake wamefanya uzembe hadi kujikuta wakiruhusu bao na kwamba wanaenda kulifanyia kazi kabla ya mchezo wao wa Ligi Kuu utakaopigwa Ijumaa jijini hapa dhidi ya Namungo.
"Waliridhika wakaamini wamemaliza mchezo wakajisahau, huu ni uzembe ambao lazima niukemee kwa nguvu wakati tukienda kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Namungo" amesema Haruna.
Naye Straika wa Mwadui, Aboubakari Malika amesema walipambana kusaka ushindi ili kusonga hatua inayofuata lakini haikuwezekana hivyo wanaenda kujipanga na mwendelezo wa Championship kuhakikisha wanaidaidia timu kufikia malengo.
"Tunakubali matokeo, tulijiandaa kupata ushindi ili kusonga hatua inayofuata lakini haijawezekana, wenzetu walipata bahati wakatumia hizo nafasi, tunaenda kujipanga upya na Championship" amesema Malika.